|
|
|
VIVUTIO VINAVYOPATIKANA NACHINGWEA
(NACHINGWEA YETU, FAHARI YETU)
ASILI YA NACHINGWEA
Nachingwea ni mji mkongwe na Makao makuu ya mji huu yalihamishiwa kutoka eneo la Ruponda hadi eneo ilipo sasa hivi. Neno Nachingwea asili yake ni mti mmoja uliokuwa ukiitwa NGWEA. Wakazi wa makao makuu ya wilaya ya nachingwea wakati huo Ruponda walikuwa wakienda kuchota maji chini ya mti wa NGWEA, kwa hiyo walikuwa wakisema NACHI NGWEA wakimaanisha naenda kwenye Ngwea, maana yake nakwenda kuchota maji kwenye NGWEA. Ndipo jina hilo Nachingwea likashika kasi na kuwa Nachingwea ya leo.
IKO WAPI NACHINGWEA?
Nachingwea kwa sasa ni mojawapo ya kati ya wilaya 6 zilizopo mkoa wa LINDI. Wilaya hii imepakana na wilaya za Ruangwa upande wa kaskazini, Lindi vijijini upande wa mashariki na mikoa ya Mtwara na Ruvuma upande wa kusini. Eneo la wilaya ya LIWALE liligawika toka wilaya ya Nachingwea mwaka 1975 na Ruangwa kutoka eneo la wilaya ya Lindi mwaka 1995. Wilaya ya Nachingwea ilikuwa Halmashauri ilipofika mwaka 1984 na ikawa mamlaka ya serikali za mitaa ambayo ilikuwa madaraka kamili kama yalivyoainishwa katika sheria ya uanzishwaji wa mamlaka izo ya mwaka 1982. Eneo la Nachingwea miaka ya 1950’s lilikuwa sehemu ya mradi wa Karanga wakati wa ukoloni wa Uingereza. Katika sensa ya 2012 jumla ya wakazi 178,464 walipatikana. Wenyeji wa Wilaya ya Nachingwea ni Wamwera, Lakini kutokana na kukua kwa jamii na kuhama hama pia utawakuta wamakonde, Wandonde, Wamakua, n.k.
RASILIMALI ZILIZOPO NACHINGWEA
Licha ya kuwepo na shughuli za Uchumi kama kilimo cha korosho, Ufuta na Mbaazi pamoja na shughuli za uchimbaji wa madini hasa Nickel, Nachingwea inajivunia kuwa mji wa UKOMBOZI katika kusaidia nchi nyingi kujikomboa na kujipatia uhuru.
UTALII ni mojawapo ya shughuli ambayo ni nguzo muhimu kwa Wilaya ya Nachingwea hasa katika kuchangia uchumi wa Taifa, wilaya na mtu mmoja mmoja. Kwa sasa Ofisi ya Utalii imejidhatiti kuleta hamasa chanya na kutangaza vivutio na fursa za utalii za Wilaya ya Nachingwea.
FURSA ZA UTALII NACHINGWEA
Nachingwea imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali ingawa bado havijetangazwa kwa kiwango cha kutambuliwa na wengi. Vivutio hivyo vipo katika makundi ya fursa za utalii wa asili (Nature), historia (History) na tamaduni ( Tradition and culture).
Nachingwea ina maeneo mengi ya asili yanayojumuisha misitu, mawe, miamba mikubwa, Machimbo ya madini, Mito pamoja na njia za Tembo ( Ushoroba). Utalii wa kutembea (walking safaris and Adventure tourism), kupiga picha (Photo taking tourism), n.k. Baadhi ya misitu pia ina wanyama wakiwepo simba, chui, ngolombwe, nyati, ngiri, nguruwe pori n.k. Wanyama hao hawaonekani mara kwa mara kwani huonekana kwa msimu au mpaka uwafuatilie (Tracing). Mawe makubwa yaliyo katika hifadhi za misitu zinaleta uhitaji wa kutembelewa pamoja na kuhifadhiwa. Baadhi ya vivutiuo hivyo ni hivi vifuatavyo:
Mji wa Nachingwea unasikika kutokana na historia yake ya ukombozi. Mji huu uliweza kuwa hifadhi ya wapigania ukombozi hususani bara la Africa kwa nchi za Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika kusini na Zimbabwe. Pia Eneo katika kata ya Matekwe liliweza kuwa eneo tengwa la wakimbizi wa kivita toka nchi ya Msumbiji. Licha ya historia ya ukombozi mji wa Nachingwea Uliweza kuwa na miradi ya karanga enzi za ukoloni na reli iliweza kuanzishwa ambayo ilikuwa inasafirisha mazao hayo kupeleka bandari ya Mtwara. Mwisho kabiasa ukifika Mji wa Nachingwea lazima utasikia vita vya Wangoni na wamwera katika milima ya Ilulu. Zifuatazo ni baadhi ya vivutio vya utalii wa kihistoria hapa Nachingwea;
Shughuli kubwa za wakazi wa Nachingwea ambao kiasi kikubwa ni Wamwera ambao hulingana tamaduni wa makabila mengi ya kusini wakiwemo wayao, wamakonde na wengine ni Kilimo cha korosho pia tamaduni hasa ngoma, jando na unyago ni mojawapo ya shughuli rasmi kwa makabila hayo maana wote hao asili yao ni kusini mwa Tanzania hususani nchi ya msumbiji. Pia kwa mtu mgeni akifika katika mji huu atashangazwa na utamaduni wa wanawake wengi kuendesha baiskeli kuliko wanaume. Pia mfumo wa wamwera ni wa mama (Matrenial parental system). Kikubwa Watu wa mji wa nachingwea hasa wamwera sifa yao kubwa ni wapenda Amani.
Mojawapo ya shughuli za kitamaduni katika mji wa Nachingwea ni hizi zifuatazo:
VIVUTIO PENDEKEZI RASMI KUMI (10) VINAVYOPATIKANA NACHINGWEA
Huu ni mlima mrefu kuliko yote katika mkoa wa lindi ambao unapatikana katika kata ya Ruponda, Tarafa ya Ruponda. Mlima huu umepewa namba moja kama Alama na kiwakilishi cha wilaya ya Nachingwea. Wenyeji wa Nachingwea ambao kwa asili ni wamwela, waliutumia mlima huu kwa ukombozi kutoka kwan uvamizi wa eneo lao ambao walikuwa ni wayao na wangoni. Wamwela waliutumia mlima huu kujificha wakati wa vita na pia walitumia mawe mazito na makubwa kuwaangamiza adui zao na kupata ushindi. Baada ya ushindi huo, walishangilia na kupiga vigeregere (Ilulu) na hivyo kuuita mlima huo ‘’Mlima Ilulu’ wakimainisha mlima wa vigeregere. Neno Ilulu ni neon la kimwela lenye maana ya vigeregere kwa Kiswahili. Mlima huu pia ulitumika kufanya matambiko ya kiasili na hivyo kulifanya eneo hili kuwa kivutio cha utalii wa kiutamaduni. Eneo la Mlima ni km 8.8 za mraba kutoka usawa wa bahari na urefunusiopungua m 900. Umbali toka eneo la mjini Nachingwea ni 20km.
Eneo hili lina vitu vifuatavyo:
Ni eneo linalojulikana kama Farm 17. Na ni eneo la kihistoria la ukombozi wa nchi za kiafrika. Palitumika kama kambi ya mafunzo ya wapiganaji nchi za Msumbiji, Namibia,Angola, Zimbwabwe, Afrika kusini.Eneo hilo ni maarufu hasa katika historia za ukombozi kusini mwa afrika hususani nchi za Msumbiji, Afrika kusini, Angola, Zimbabwe, Namibia na Msumbiji. Eneo hili Raisi wa Tanzania alitenga kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi kwa nchi hizo. Ni umbali wa km 30 kwa gari tokea mjini Nachingwea.
Eneo hili kuna majengo ya kumbukizi kama vile:
Pia eneo hili kwa kuwa watu wa msumbiji walikaa kwa muda mrefu, eneo hili hasa hujulikana kama eneo la msumbiji au Samora machel ambaye alikuwa mkuu wa kambi na baadaye kuwa mwenyekiti wa Frelimo baada ya kuuliwa kwa kiongozi mwanzilishi Eduado Mondlane na baadaye kuwa raisi wa kwanza wa Msumbiji. Pia Samora machel aliishi katika nyumba ambayo ipo katika eneo hilo iliyokamilika mwanzoni mwa miaka ya 70’s.
‘Katika kata ya kipara mtua, Tarafa ya Naipanga ndiko linapatikana eneo la farm 17. Mwanzo kabisa eneo hili lilianza kama kambi kwa wapigania uhuru wa Flerimo- Msumbiji. Baada ya Askali wa Frelimo kukaa kwa muda majengo ya kambi hii yalitumika kama chuo cha kufundishia wanajeshi. Chuo hiki kilikuwa kinatoa mafunzo kwa maafisa kwa jeshi kutoka nje ya nchi pamoja na mafunzo ya awali kwa askali wanaoanza. Nchi zilizoleta askari wake kupata mafunzo ni pamoja na Msumbinji, Zimbabwe na Angola hadi pale zilipopata uhuru. Mnamo mwezi desemba 1992 chuo hiki kilivunjwa na kuhamishiwa Mgulani Dar es salaam. Eneo hili ni kivutio kizuri cha wilayani hapa’’ Mwl Longnus Nambole – Mwalimu mkuu wa kwanza wa sekondari ya Farm 17.
Eneo hili lipo tarafa ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea na ni eneo lenye historia kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na watu wa Msumbiji. Ni km 110 kufika eneo hilo tokea Nachingwea mjini.
HISTORIA YA ENEO
Kwa historia ya hivi sasa iliyowasilishwa na mkazi wa Matekwe mzee Salumu Mohamed Migomba (Mei, 2021). ‘’ Anasema watu walianza kuja hapo kwa kuletwa na serikali mwanzoni mwa miaka ya 1960’s. Watu walianza kujenga mji hadi pale miaka ya 1967 alipofika waziri mkuu wa Tanzania wakati huo Mzee Mfaume kawawa kuwaomba wananchi kuwapokea wageni ( Wakimbizi tokea nchi ya Msumbiji ambao wapo katika mapigano ya ukombozi). Wakimbizi wasiopungua 15,000 walifika eneo la matekwe na kutawanywa katika maeneo mbalimbali yaliyoitwa barabara.’’
MAJENGO YALIYOJENGWA KWA AJILI YA WAKIMBIZI.
Ukifika eneo la Matekwe utakayakuta majengo tofauti ambayo yalitumiwa na wakimbizi, viongozi na majengo ya shughuli za jamii wakati huo ambayo hadi sasa yanaendelea kutumiwa kama ofisi za kijiji, zahanati, kanisa, shule n.k. Majengo hayo ni:
KUONDOKA KWA WAKIMBIZI NA URITHI ULIOACHWA
Baada ya Nchi ya msumbiji kupata uhuru mnamo tarehe 25. 06. 1975. Serikali yao ilitangaza wakimbizi wote kurudi nchini humo. Wengi walirudi japo inasemekana wengine waliishia njiani na kuanzisha makao mapya na wengine walichanganyika na wanajamii wengine kusini mwa Tanzania. Pia majengo yote yaliachwa na serikali ya Tanzania iliamua kuyahifadhi maeneo hayo kwa kuendeleza huduma zilizokuwa zinatolewa. Hivyo ukiende leo eneo la matekwe utapata historia ya eneo hilo kwa uzuri.
Jiwe ni kivutio tosha wilayani na kuna historia ya Jiwe hilo linaloaminika palikuwa ni sehemu ya matambiko mfano kama mvua hainyeshi na baada ya kufanya matambiko wakishuka chini yam lima(jiwe) basi mvua hunyesha. Kwa sasa pamejengwa kanisa la biblia ambalo lilijengwa miaka ya 1991. Pia wanajamii wanaamini eneo hilo kulikuwa na joka kubwa ambalo lilikua linatoka nje na kurejea kwenye shimo na inaaminika liliuawa na mzungu ambaye alifika eneo hilo na kuwekeza. Kwa taarifa za msimamizi wa eneo hilo anasema eneo hilo walinunua na kujenga kanisa la biblia na lilikuwa na nyoka wa kawaida waliotumika kama ulinzi katika mashamba ya karanga. Nyoka hao walikuwa wanakula panya. Pia eneo hilo Askari wa kjeshi walitumia kama eneo la mafunzo ya makombola na mabomu na inasemekana Waziri Kawawa alitaka kudunguliwa kwa sababu alifika bila taarifa. Eneo hili lina mapango ambayo mengine yamegeuka kuwa vyoo na majengo ya kanisa na jiwe kubwa. Ni eneo nzuri kwa uwekezaji. Ni eneo tulivu ambalo watu wengi hutembelea hususani wakati wa mapumziko na sikukuu.Ni mwendo wa km 1.5 toka eneo la mjini.
Eneo la Kilimarondo limetawaliwa wenyeji ambao ni kabila la WA NDONDE na shughuli za utalii zinaweza fanyika pia hususani utalii wa picha, kuona mapango ya popo, kupanda mlima n.k. Ni mwendo wa km 100 tokea eneo la Nachingwea mjini.
Mji wa Kilimarondo ulianza miaka ya 1939 na ulishamiri baada ya ujio wa Askofu Joachim aliyesindikizwa na DC kwa ajili ya kujenga kanisa(Mission). Askofu aliwahita wazeee Maarufu na mashuhuri akiwemo mzee ALI Machemba, Mnawa na mwenye Kamila na kuomba kuoneshwa eneo la ujenzi la kanisa na alioneshwa eneo ambalo lilikuwa na wanyama wakali kama Simba na tembo ili aweze kuondoka ila cha ajabu eneo hilo Askofu alipendezwa nalo na ndipo ujenzi ulifanyika wa mission ambayo iko hadi sasa na ikapelekea kukua kwa eneo hilo.
Uoto wa asili uliopabwa na milima ya Kilimarondo ambayo ina historia yake , kabla ya kuitwa kilimarondo ilijulikana kama milima ya Lilondo. Milima hii ndio asili ya kata na kijiji pia safu ya milima ambayo imejipanga ambayo ina historiaa pia kuna mapango ya popo ambao huzalisha kinyesi ambacho watu hutumia kama mbolea. Inasemekana inachukua masaa 6 kufika kileleni.
Ukifika Eneo la Ruponda utaacha kusikia jina la mzee Nakotyo aliyekuwa kiongozi wakati wa uvamizi wa wangoni miaka ya 1896. Kwa kuwa alikuwa Mkulungwa wa eneo hilo aliwaongoza wamwera hususani katika mipango ya kukimbilia mlima Ilulu. Kaburi la Mzee huyu lipo eneo la Ruponda ambalo liko chini ya familia. Kwa sasa mambo ya mila anasimamia mjukuu wake anayejulikana kama Nakotyo 5. Umbali tokea mjini Nachingwea ni km 20.
Eneo hili lipo karibia na makao makuu ya wilaya hivi sasa ambapo ofisi nyingi za utawala zipo hapa Pia kaburi hili liliopo katika eneo hili linafanya eneo liwe na umaarufu sana.Wageni toka nchi jirani kama afrila kusini huja kuangalia kaburi hili.
Historia ya Mbwa huyu anayeitwa ‘JUDY” likimaanisha ‘Peace” (Amani) aliyezaliwa February 1936 china, na baadaye kuchukuliwa na vikosi vya kivita vya majini zaidi ya miaka 6 kabla ya kuja afrika mashariki eneo la Nachingwea, Lindi. Judy alitunukiwa medali za kijeshi nyingi. Mwaka 1950 alifariki chini ya uangalizi ya Mr Frank wiliams ambaye alikuwa naye muda wa vita na alikuja naye Nachingwea katika kusimamia mradi wa karanga(Groundnut scheme). Wakazi wa Nachingwea waliokuwa wanahudumia mashamba watamkumbuka sana ‘Judy’ kwa utumishi wake na masaada wake na huduma zake hususani kwa Mr Frank. Baada ya kufariki katika hospitali ya wilaya Nachingwea alizikwa karibu na eneo la mmiliki mr Frank wiliams na alijengewa kaburi na kuwekwa maneno ya ukumbusho juu yake. Kutokana na umahiri wake wa mapambano vitani hususani vita vya pili vya dunia , Mbwa huyu licha ya kupewa medali alipewa pia cheo cha kijeshi na kutambulika kama Brigedia. Baada ya kifo chake wakati wa vita, mbwa huyu alizikwa kwa heshima zote za kijeshi na kaburi lake lipo mpaka leo.
Makala ya historia ya Judy inapatikana katika kitabu kinachoitwa ‘THE JUDY STORY – The Dog with six Lives, E VARLEY(1973)
Hazina hii ipo katika msitu wa Lionja.Utalii ndani ya msitu (Maliasili) ni muhimu sana kwani msitu huu umejawa na uoto wa asili, pamoja na jiwe kubwa la asili ambalo Ndio laweza kuwa kubwa katika Nachingwea. Jiwe hili lina urefu usiopungua mita 200 na ili uweze kupanda unatakiwa usiwe na nia ovu na inabidi wazee wa kijiji watambue uwepo wako. Pia wazee walitumia jiwe hilo kwa kutambikia. Umbali kutoka Nachingwea mjini hadi eneo hili ni km 40.
Katika ukanda wa Nachingwea eneo la Mbondo na maeneo karibu kuna hifadhi hiyo. Katika uhifadhi wanyamapori imeanzishwa jumuiya ya uhifadhi iitwayo NDONDA ambayo ipo katika hatua za kuombewa hati ya usajili kuwa jumuiya ya Jamii iliyoidhinishwa pamoja na kupatiwa haki ya matumizi. Jumuiya hiyo ina ukubwa wa hekta 75,353.90 na ipo katika Wilaya mbili za Nachingwea na Nanyumbu. Uhifadhi jamii shirikishi kwa Wilaya ya Nachingwea ni dhana inayotumika katika kuhifadhi misitu ya asili ili kuboresha ikolojia ya mimea na wanyama. Vijiji vilivyopitiwa na jumuiya hiyo Upande wa Nachingwea ni Mbondo, kilimalondo, Majonanga, Matekwe, Mtua, Nahimba, Chimbendenga,
Eneo hili lina mabaki ya njia za reli, gereji pamoja na nyumba za wafanyakazi na nyumba ya wageni. Reli hiyo ilikuwa inabeba mazao ya karanga kupeleka sehemu zingine ikiwepo mtwara banadarini kabla ya mradi wa karanga kuachwa. Eneo hili liko Kata ya stesheni. Umbali wa km 3 toka mjini Nachingwea.
MALAZI NA CHAKULA
Nachingwea ina nyumba za wageni zinazojitosheleza kwa gharama nafuu. Chakula pia kinapatikana katika migahawa ya asili, migahawa ya kisasa na baadhi ya nyumba za wageni(Lodges) zinatoa chakula pia.
USAFIRI NA MIUNDOMBINU
Nachingwea ina uwanja wa ndege ambazo ndege zinaweza kutua. Pia usafiri wa Mabasi toka mikoani hususani kutokea Dar es salaam, mtwara na masasi unapatikana kila siku. Maeneo tajwa yanafikika kwa barabara za changarawe na maeneo mengine yanahitaji maboresho madogo madogo.
Imeandaliwa na Ofisi ya Utalii,
Idara ya Maliasili
Nachingwea
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.