Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, Dkt. Ramadhan Mahiga, amesema hospitali imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi baada ya kununua mashine mpya ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 40, Amesema ununuzi huo ni sehemu ya mikakati ya hospitali katika kuimarisha miundombinu ya huduma za uchunguzi wa magonjwa na kuongeza ufanisi wa matibabu.
Akizungumza ofisini kwake, Dkt. Mahiga amesema kuwa mashine hiyo ni maalum kwa ajili ya kupima figo, ini na kiwango cha mafuta mwilini ina uwezo wa kupima hadi sampuli 100 kwa saa moja, Teknolojia hiyo mpya itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo, hivyo kuruhusu wagonjwa kuanza matibabu mapema na kuboresha huduma za afya kwa ujumla.
Dkt. Mahiga ameongeza kuwa uwepo wa mashine hiyo utarahisisha upimaji wa sampuli nyingi zaidi kwa wakati mmoja, hatua ambayo itapunguza msongamano wa wagonjwa maabara na kuongeza ufanisi wa watumishi, Aidha, alisema kuwa hospitali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea na Wizara ya Afya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Kemia katika maabara ya hospitali, Bw. Feisal Munu, ameipongeza Serikali pamoja na Halmashauri ya Wilaya kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuhakikisha hospitali inapata vifaa vya kisasa, Amesema mashine hiyo imeleta mapinduzi makubwa kwani sasa majibu ya vipimo hupatikana ndani ya saa moja pekee, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo majibu yalichukua hadi masaa 24 kutokana na uwezo mdogo wa mashine iliyokuwepo.
Bw. Munu amesisitiza kuwa teknolojia hiyo itachangia kuongeza ubora wa huduma za uchunguzi na kutoa majibu sahihi kwa muda mfupi, Pia amewahimiza wananchi wa Nachingwea na maeneo jirani kuendelea kujitokeza kupata huduma katika hospitali hiyo, akisema kuwa uboreshaji huu ni ishara ya dhamira ya Serikali katika kuimarisha huduma bora za afya kwa wote.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.