Katika kuboresha huduma za afya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Daktari Samia Suluhu Hassan imejenga jengo jipya la Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, hatua hii inatajwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo na maeneo jirani, kwani inalenga kuinua ubora wa huduma za afya na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za mbali.
ICU ya zamani
Jengo hili jipya la ICU limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 250, huku shilingi milioni 383 zikitumika kununua vifaa tiba vya kisasa vinavyokidhi viwango vya kimataifa pia kiasi cha shilingi milioni 9.25 zilitumika mahususi kwa ajili ya mafunzo maalumu ya wataalamu watano wa afya wanaotoa huduma katika kitengo hicho ambapo walipatiwa mafunzo hayo katika Hospitali ya Taifa ya Mhimbili.
Mradi wa ujenzi wa jengo hili ulianza rasmi Machi 11, 2022 na kukamilika Septemba 30, 2022, Hii ni ishara ya dhamira ya serikali na uongozi wa Wilaya kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wakati bila kucheleweshwa na changamoto za miundombinu au vifaa duni.
Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa mahututi 10 kwa wakati mmoja, wakiwemo watoto, limezingatia mahitaji maalum ya kuhudumia wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko yanayoambukiza kama vile COVID-19 na Mpox, kwa kujumuisha chumba maalumu vya kuzuia maambukizi (Quarateen)
Uwepo wa ICU hii ya kisasa imekuwa faraja kubwa kwa wakazi wa Nachingwea na wilaya jirani, kwani sasa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum hawalazimiki tena kusafirishwa hadi hospitali za Ndanda na Sokoine au maeneo mengine ya mbali, hali hii imepunguza gharama za matibabu na usafiri, huku ikihakikisha huduma za dharura zinatolewa haraka na kwa ufanisi.
ICU mpya ya Nachingwea imefungwa vifaa vya kisasa kama mashine za kusaidia upumuaji (ventilators), vifaa vya ufuatiliaji wa hali za wagonjwa (monitors), na mifumo ya uhifadhi wa mitungi ya gesi ya oksijeni, Vifaa hivi vimepunguza kwa kiasi kikubwa athari zinazoweza kujitokeza wakati wa matibabu ya dharura na kuhakikisha wagonjwa wanapokea huduma bora kila wakati,
Kabla ya ujenzi wa jengo hili, hospitali ilikuwa na wodi ndogo ya wagonjwa mahututi iliyoweza kuhudumia wagonjwa watatu pekee, Hali hiyo ilisababisha changamoto kubwa wakati wa ongezeko la mahitaji ya huduma za dharura, hususan wakati wa milipuko ya magonjwa, Uwepo wa jengo jipya sasa ni suluhu ya kudumu kwa changamoto hizo.
Zaidi ya kutoa huduma bora, jengo hili limekuwa kituo muhimu cha mafunzo kwa wanafunzi wa taaluma za afya kutoka ndani na nje ya wilaya, wanafunzi wa fani mbalimbali za kitabibu sasa wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo katika mazingira yenye vifaa na teknolojia ya kisasa.
Wananchi wa Wilaya ya Nachingwea wameeleza furaha na shukrani zao kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Daktari Samia Suluhu Hassan na uongozi wa wilaya kwa kutambua changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo kwa muda mrefu pia wamepongeza juhudi za kuhakikisha huduma za afya za kiwango cha juu zinapatikana karibu na bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za ICU.
Ujenzi wa jengo jipya la ICU katika Hospitali ya Nachingwea unatajwa kuwa ushuhuda wa dhamira ya serikali kuboresha sekta ya afya nchini, Mradi huu ni mfano bora wa ushirikiano kati ya serikali, wataalamu wa afya na wananchi, na unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo zaidi katika huduma za afya, si tu Nachingwea bali pia kwa mikoa jirani.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.