Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Mhandisi Chionda M. Kawawa amesema hana nia ovu na wafanyabiashara wa Nachingwea bali yupo tayari kuhakikisha ustawi wao wa kibiashara, amewasihi wafanyabiashara hao kuacha maneno ya barabarani na kusisitiza kukaa mezani na kufikia muafaka.

Mhandisi Kawawa ameyasema hayo leo Januari 6, 2026 katika mkutano na wafanyabiashara ulioitishwa na mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mh.Fadhili Liwaka katika ukumbi wa Singapore.

Katika mkutano huo wafanyabiashara wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw. Rashidi Kassimu waliwasilisha hoja kadhaa zikiwemo kukosa fursa za kibiashara kwenye miradi ya serikali, madeni ya muda mrefu ya wazabuni, malalamiko juu ya makadirio ya kodi na mgogoro wa umiliki wa vibanda na ardhi katika soko kuu ambao wafanyabiashara hao walidai kuna nia ovu juu yao.

Akijibu hoja hizo Mhandisi Chionda alisema, "kuhusu suala la vibanda mimi nalielewa na kweli lipo kihistoria na mimi naliheshimi hilo, hakuna mwenye nia ovu hapa,nawasihi sana tuache maneno ya barabarani tukae mezani,mimi ndio mkurugenzi nawaambia hakuna haki ya mtu itakayopotea".

Aidha kwa upande mwingine Mhandisi Chionda amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa kuanzia Januari hii madeni yote kama sio kumaliza kabisa basi atahakikisha anayapunguza.
Aliongeza kusema kuwa tangu amekuja Nachingwea mwaka 2021 alikuta madeni ya zaidi milioni 400 ambayo hayakuwa na vielelezo.Akasema kuwa moja ya hatua aliyochukua ni kuhakiki madeni yote ili yaweze kulipika,hali ambayo inaonesha nia yake njema Kwa wafanyabiashara hao.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.