Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo, amewataka madiwani kuwa kichocheo cha maendeleo kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi, Pia amesisitiza kuwa wana wajibu wa kuwakimbilia wananchi, kusikiliza changamoto zao na kutoa ahadi zinazotekelezeka kwa lengo la kuleta maendeleo chanya katika maeneo yao.

Ameyasema hayo leo januari 8, 2026 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya za Nachingwea na Liwale yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.

Mheshimiwa Moyo amesema mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia Madiwani kuwa viongozi bora, wazalendo na wenye uwezo wa kutatua kero za wananchi kwa ufanisi. Ameongeza kuwa maarifa yatakayopatikana kupitia mafunzo hayo yanapaswa kutumika moja kwa moja katika kuwahudumia wananchi na kuboresha ustawi na maendeleo kwa jamii.

Aidha, amewahimiza Madiwani kuwa wasikivu, waadilifu wa karibu na wananchi ili kujenga imani na mshikamano wa kudumu. Pia Mkuu wa Wilaya amewapongeza na kuwashukuru waandaji wa mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kuongeza ujuzi wa uongozi kwa madiwani.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuweka mkazo katika mshikamano kati ya viongozi na wananchi, ikijengwa juu ya misingi ya uzalendo, utu, uwazi, umoja na uwajibikaji.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.