Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea imefanya maboresho ya vifaa vya kutolea huduma za maabara kwa kununua vifaa vipya kama vile mashine ya kemia yenye thamani ya milioni 40 ambayo inauwezo wa kupima vipimo za sampuli 100 za magonjwa kwa saa 1 ambapo kabla ya maboresho hayo baadhi ya vipimo kama elektroraidi ambayo haikuwa na kipimo ilipelekea kutolewa rufaa kwenye hospitali za Ndanda, Nyangao na Muhimbili kwa wagonjwa wa kisukari kwa matibabu yao ya dharura.

Wakizungumza na mwandishi wetu, Bi. Stella Francis na Ndugu Bakari Abdallah wagonjwa waliopata vipimo katika maabara hiyo wamesema wakati huu wanapata huduma bora tofauti na awali hivyo kumepunguza adha ya kutoka na kwenda hospitali zingine kupatiwa matibabu.

Nae Ndugu Feisal Mnoha Meneja wa Maabara ya hospitali hiyo amesema maboresho ya vifaa yamewarahisishia wataalamu kazi lakini pia kuweza kuwasaidia wagonjwa kupata huduma kwa wakati kwa maana ya mashine ya mwanzo ilikuwa inahitaji mwongozaji ili iweze kufanya kazi lakini baada ya kupokea mashine mpya inaweza kufanya kazi bila mwongozaji.
Kwa upande wake Dkt. Shukrani Nsikini Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Nachingwea amesema kuboreshwa kwa vifaa vya maabara kumeongeza wigo wa utowaji wa huduma za kitabibu "tumenunua mashine ya kemia yenye thamani ya milioni 40 ambayo inapima vipimo vingi sana na kwenye hivyo vipimo pia vipo vipimo vilivyokuwa havipimwi hapo awali lakini kwa sasa tunafanya na imesaidia kupunguza rufaa zisizo za lazima". Dkt. Nsikini alieleza.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.