Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mheshimiwa, Hashim Komba amewataka wananchi wa wilaya ya Nachingwea kutogawanywa na sababu za uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019.
Akiongea na wananchi wa Mkotokuyana jana aliwataka wale ambao hawajaridhika na mchakato huo kufuata sheria na kanuni za uchaguzi ambazo zinaelekeza kukata rufaa na kuweka mapingamizi kwa mujibu wa maelekezo ya Uchaguzi mwaka 2019.
“Kazi kubwa ya siasa ni kuleta maendeleo si malumbano, tutumie fursa za kisheria tusibaki kulalamika, uteuzi ukishafanyika pingamizi linawekwa kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kama hujaridhika unakata rufaa kwa kamati ya rufaa wilayani” aliongeza Mheshimiwa Koma.
Ameyasema hayo kufuatia swali liloulizwa na ndugu, Amani Lalo akitaka kujua sababu za baadhi ya wagombea kutoteuliwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji.
Aidha, akiongelea malipo ya korosho amewataka wananchi kuwa wavumilivu huku michakato ya kuwalipa ikiwa inaendelea kwani watalipwa hivi karibuni.
“Serikali ni kumlinda mkulima ili apate haki yake na si kupambana nae, korosho ndio utajiri wa Nachingwea, Lindi, Mtwara na Pwani, Wilaya yetu wakulima wanadai shilingi Bilioni 3.4 ambazo Rais ameelekeza zilipwe na zitalipwa hivi karibuni” Aliongeza Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya yupo kwenye ziara yake yenye nia ya kujitambulisha na kusikiliza kero za wananchi wa wilaya ya Nachingwea
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.