Wananchi wafurahia upanuzi wa kituo cha Afya Kilimarondo
Wananchi wa Tarafa ya Kilimarondo wameishukuru na kuipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe magufuli kwa kuleta fedha kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha afya Kilimarondo
Waliyasema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Godfreya Zambi alipofanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya katika kituo hicho cha Afya jana , kilichopo takribani Kilomita 90 kutoka Nachingwea mjini.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais John Magufuli kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo haya, kwani isingelikuwa yeye tusingepata majengo haya yatakapokamilika yatatusaidia sana” Alisema Ephrostina Jastin
Naye ndugu Salum Pilikano amesema kwa mda mrefu Kituo cha afya Kilimarondo kimekuwa hakina huduma za upasuaji lakini wanaamini mara baada ya kukamilika kwa kituo hicho huduma hizo zitakuwa zikipatikana katika maeneo hayo na hivyo kupunguza gharama za kupata huduma za afya.
Wananchi hao wamedai kuwa baada ya kukamilika kwa kituo hicho vifo vya mama na mtoto vitapungua kwani kutokana na umbali wakina mama wamekuwa wakijifungulia njiani na nyakati zingine wamekuwa wakifariki kutokana umbali kutoka Kilimarondo hadi ilipo hospitali ya Wilaya.
Aidha Mkuu wa Mkoa ameipongeza Halmashauri kwa usimamizi mzuri hadi mradi ulipofikia, na kutaka usimamizi uendelee ili kukamilisha mradi huo kwani umaliziaji usipokuwa mzuri kazi ya ujenzi wa majengo hayo utakuwa hauna maana.
“Katika hatua hii huwezi kuona dosari, tuongeze usimamizi kwenye ‘finishing’ kwani mafundi wengi wanapata shida sana kwenye hatua hizi” Alisema Mheshimiwa Zambi.
Kituo cha Afya Kilimarondo ni miongoni mwa vituo vituo vya afya nchini vilivyopewa Shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ya kutolea huduma, ambapo katika kituo hicho majengo ya jengo la maabara, jengo kujifungulia mama wajawazito, jengo la upasuaji na jengo la kufifadhia maiti yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.