Tarehe 26 Aprili 2025, hafla fupi ya chakula cha jioni iliandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Sita wa Nachingwea High School na Rugwa Boys, wanaotarajia kuanza mitihani yao ya kitaifa tarehe 5 Mei 2025.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na elimu, ambapo mgeni rasmi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Mheshimiwa Adinan Mpyagila. Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Mwenyekiti amewatakia wanafunzi mitihani yenye mafanikio na kuwasisitiza kuendeleza viwango vya ufaulu vinavyoifanya Nachingwea High School kuwa miongoni mwa shule bora.
Aidha, amewahimiza wanafunzi wa Rugwa Boys kufanya vizuri kwa kuwa wao ndio kundi la kwanza la wahitimu wa shule hiyo, ambayo imejengwa kwa fedha za wananchi kupitia kodi ya zao la korosho. Amesisitiza kuwa mafanikio yao yatafungua historia mpya na kuongeza hamasa kwa wanafunzi wanaofuata.
Mheshimiwa Mpyagila pia amewapongeza walimu kwa juhudi na kujitolea kwao katika kukuza taaluma na kuongeza heshima ya wilaya. Alieleza kuwa ufaulu wa wanafunzi unaongeza mvuto wa shule hizo na kuwavutia wazazi wengi kupeleka watoto wao huko.
Kwa upande wao, wanafunzi walitoa shukrani kwa walimu na uongozi wa shule kwa kuwaandaa kwa moyo wa upendo na kujitolea. Waliahidi kufanya vizuri katika mitihani yao kwa lengo la kupata daraja la juu.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa sala na dua za kuwaombea wanafunzi mafanikio mema katika safari yao ya kitaaluma.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.