Leo tarehe 6 Julai 2025, Wakulima wa zao la Ufuta kupitia Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI Ltd kutoka Wilaya ya Nachingwea wameendelea kuonesha mwitikio mzuri kwa mfumo wa uuzaji wa mazao kupitia minada rasmi, baada ya kuridhia kuuza Ufuta katika mnada wa nne uliofanyika katika ghala la Marambo Amcos, wilayani Nachingwea.
Mnada huo umeandaliwa na RUNALI Ltd, Chama Kikuu cha Ushirika kinachoshirikisha Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata bei yenye tija kupitia ushindani wa wazi sokoni.
Katika mnada huo, bei ya juu ya Ufuta imefikia shilingi 2,630 kwa kilo, huku bei ya chini ikiwa ni shilingi 2,550 kwa kilo. Jumla ya kilo 5,234,770 za Ufuta zimeingizwa sokoni, na wakulima kupitia RUNALI Ltd wameridhia kuuza kwa bei hizo, jambo linaloashiria mwamko chanya na matumaini mapya ya kiuchumi kwa wakulima hao.
Sambamba na hilo, mnada wa kwanza wa zao la Choroko pia umefanyika ambapo tani 8 na kilo 636 zimeuzwa kwa bei ya shilingi 1,310 kwa kilo. Hili linaashiria kuwa mazao mbadala nayo yanaanza kupata nafasi katika masoko ya ushindani, hivyo kusaidia kuongeza kipato kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.