Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Lindi wamepatiwa mafunzo mbalimbali ya kitaalamu katika kipindi cha maonesho ya madini yaliyofanyika hivi karibuni, kwa lengo la kuboresha shughuli zao na kuongeza thamani ya madini wanayochimba.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Zainab Telack, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wachimbaji kuelewa mabadiliko ya kiteknolojia katika sekta ya madini pamoja na kuimarisha usalama, uzalishaji, na uendeshaji wa shughuli kwa kufuata sheria Mafunzo yaliyotolewa yalijumuisha elimu ya Sheria ya Madini (Sura ya 123), ambapo Tume ya Madini ilitoa elimu kuhusu umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria, kupata leseni halali, utunzaji wa mazingira, na kushirikiana kwa uwazi na serikali.
Mada nyingine muhimu ni kuhusu usalama migodini na usimamizi wa baruti, ambapo wachimbaji walielekezwa kuhusu matumizi salama ya baruti kwa kufuata sheria na miongozo ili kuepusha ajali migodini.
Aidha, taasisi za kifedha ziliwasilisha taratibu za utoaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo, jambo ambalo linatoa fursa ya kuwapata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao kwa tija.
Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ilitoa mafunzo kuhusu matumizi bora ya kemikali migodini, kwa lengo la kulinda afya za wachimbaji na mazingira. Wachimbaji walielekezwa kuhusu hatari za matumizi holela ya kemikali na jinsi ya kushughulikia kwa usalama
Mheshimiwa Telack alisisitiza kuwa elimu hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha wachimbaji wanajengewa uwezo wa kitaalamu na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.