Leo tarehe 14 Mei 2025, Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea imeendesha mafunzo ya siku moja kwa Waendesha Vifaa vya BVR (Biometric Voter Registration) na Waandishi Wasaidizi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya uboreshaji awamu ya pili ya uandikishaji.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa shule ya Nachingwea Day na yamefunguliwa rasmi na Afisa Mwandikishaji Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Chionda Kawawa. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhandisi Kawawa amewataka washiriki wote kuzingatia kiapo walichoapa kwa dhamira ya kweli, kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo kwa taifa.
“Tumepata dhamana hii kubwa ya kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa anapata nafasi ya kuandikishwa. Hili ni jukumu la kitaifa, hivyo ni lazima tulitekeleze kwa uaminifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema Mhandisi Kawawa.
Afisa Mwandikishaji pia amesisitiza umuhimu wa teknolojia ya BVR katika kuhakikisha usahihi na ufanisi wa mchakato wa uandikishaji, akieleza kuwa matumizi sahihi ya vifaa hivyo ni msingi wa kuwa na daftari la kisasa, sahihi na linaloaminika.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo washiriki katika kutumia vifaa vya BVR kwa usahihi, kuelewa taratibu za uandikishaji pamoja na namna ya kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Aidha, Halmashauri ya Nachingwea inatoa wito kwa wananchi wote wenye sifa za kuandikishwa, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura ambalo litaanza rasmi tarehe 16 Mei hadi 22 Mei 2025, wananchi wanakumbushwa kufika katika vituo walivyojiandikisha awali kukagua taarifa zilizobandikwa katika vituo hivyo. Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.