Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, amezindua rasmi awamu ya tatu ya mradi wa Timiza Malengo, utakaotekelezwa katika Mikoa 10 na Halmashauri 36 nchini kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ummy alisema kuwa mradi huu unalenga kupambana na maambukizi ya VVU kwa vijana , hasa walio mashuleni na wale walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu. Mradi huo utaongeza ufanisi wa elimu ya kujikinga na VVU, huku ukilenga kuwakwamua kiuchumi vijana katika mikoa ya Singida, Lindi, Morogoro, Njombe, Dodoma, Tabora, Tanga, Ruvuma, Geita, na Mara.
Aidha, Mhe. Ummy alisisitiza kuwa Tanzania imefanya maendeleo makubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI, ambapo maambukizi mapya yamepungua kutoka 100,000 hadi 60,000 mwaka 2023. Alieleza kuwa asilimia 90 ya watu walio na VVU wanatumia dawa za kufubaza virusi, na vifo kutokana na UKIMWI vimepungua kutokana na uboreshaji wa huduma na tiba.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Catherine Joachim, alieleza shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kutekeleza mradi huu, akisema kuwa utawafikia vijana balehe walioko katika hatari kubwa ya maambukizi ya VVU. Dkt. Catherine aliongeza kuwa mradi huu utachangia kufikia malengo ya kimataifa katika mapambano dhidi ya UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Kwa kumalizia, Dkt. Catherine alisisitiza umuhimu wa jitihada za makusudi kutokomeza UKIMWI, akimpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kuhimiza mapambano dhidi ya ugonjwa huu.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.