Diwani wa Kata ya Mpiruka, Mheshimiwa Veronika Makotha, Februari 11, 2026 ametoa zawadi kwa shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa ya Darasa la Nne, Darasa la Saba, Kidato cha Pili na Kidato cha Nne. Zawadi hizo zimejumuisha fedha taslimu, vyeti, sukari na mahindi kilo 200 kwa kila shule kama njia ya kuongeza hamasa kwa walimu na wanafunzi.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Shule ya Sekondari Mpiruka, Mhe. Makotha amesema amehamasishwa na umuhimu wa elimu katika maendeleo ya jamii, na kusisitiza kuwa motisha hiyo itasaidia kuongeza juhudi katika ufundishaji na ujifunzaji.

Aidha, amewataka wazazi na wadau wa elimu kushiriki kikamilifu katika kuchangia chakula mashuleni, akieleza kuwa lishe bora huchangia ufaulu wa wanafunzi. Pia aliwataka wenyeviti wa vijiji na walimu wakuu kusimamia zoezi hilo kwa umakini.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata, Ndugu Boniface Ayoub, amesema ufaulu umeongezeka ukilinganisha na miaka iliyopita licha ya changamoto ya uchangiaji wa chakula. Wazazi na wanafunzi wameahidi kuendelea kushirikiana ili kuimarisha sekta ya elimu na kudumisha mafanikio hayo.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.