Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Lindi imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo na hatua mahususi zinazochukuliwa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa kamati hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani Nachingwea, ziara hiyo imeongozwa na Katibu wa Siasa wa Mkoa wa Lindi, Ndugu Barnabasi Essau.

Katika ziara hiyo, kamati ilikagua miradi mitatu mikubwa ikiwemo ujenzi wa Jengo Jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, ujenzi wa Barabara ya KKKT kuelekea Hospitali ya Wilaya, pamoja na ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi na Awali katika eneo la Shule ya Sekondari Stesheni.

Miradi hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.6 ipo katika hatua za ukamilishaji, jengo jipya la utawala limefikia asilimia 80 ya utekelezaji na linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni tatu, Barabara ya KKKT yenye urefu wa kilomita 0.5 imegharimu shilingi milioni 356, huku ujenzi wa shule ya msingi na awali ukiwa katika hatua za mwisho kwa gharama ya shilingi milioni 314.
Akizungumza mbele ya wananchi wa eneo la Stesheni, Ndugu Essau alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo pamoja na timu ya wataalamu wa halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Mhandisi Chionda M. Kawawa kwa kutekeleza Ilani ya Chama kwa ufanisi.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, niwashukuru na kuwapongeza wewe pamoja na timu ya wataalamu kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Tumetembelea miradi mitatu ambayo ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji, hivyo nitoe wito ikamilike kulingana na ratiba iliyopangwa,” alisema Essau.
Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa walieleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na uongozi wa halmashauri, wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.