Leo tarehe 28 kimefanyika kikao kazi cha maandalizi ya msimu wa ununuzi wa mazao ya ufuta na mbaazi kwa mwaka 2025/2026 katika ukumbi wa shule ya St. Walburga, kwa Chama Kikuu cha Ushirika Runali.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Mohamed Hassan Moyo, amesisitiza umuhimu wa ubora wa mazao, akionya kuwa vyama vitakavyopokea mazao yasiyo na viwango vitachukuliwa hatua kali. “Lazima tujipambanue kwa ubora; tuendelee na viwango tulivyonavyo. Watu wanaopanga kuchanganya makapi na mazao, wazo hilo lifutwe,” amesema.
Amehimiza uadilifu, uaminifu na uzalendo kwa viongozi wa ushirika na kuwataka kuwa daraja bora kati ya wakulima na masoko. Pia amesisitiza malipo ya haraka kwa wakulima. “Mkuli wa mnada wa kwanza asilipwe kwenye mnada wa tatu tuache ujanja ujanja,” amesema kwa msisitizo.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Mkoa wa Lindi, Bw. Keneth Shemdoe, ameelekeza vyama 43 ambavyo bado havijapitisha bajeti zao kukamilisha ndani ya siku 14. “Viongozi watakaoshindwa kutimiza wajibu wao, watupishe,” amesema.
Mwenyekiti wa Runali Odas Mpunga amepongeza AMCOS kwa kazi nzuri, akiwataka kufanyia kazi maelekezo yote waliyopewa. Pia amepongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo na kuahidi kuwa wanaushirika wataitumia kama nyenzo ya kuleta mafanikio zaidi kwa wakulima.
#Tupovizuri
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.