Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bi Zuwena Omary leo June 17, 2025 amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kutenga 20% kutoka katika mapato yatokanayo na mazao na kuipatia idara ya kilimo kwa ili kuboresha utendaji kazi wa idara hiyo na kuongeza uzalishaji utakaopelekea kuongeza mapato zaidi kwani asilimia kubwa ya mapato ya halmashauri yanatokana na kilimo.
Katibu Tawala ameeleza kuwa, kwa kiasi kikubwa Halmashauri za Mkoa huo zinategemea kilimo kama chanzo kikubwa cha mapato hususani Halmashauri ya Nachingwea, hivyo ni vizuri idara hiyo kuwezeshwa ili kuiongezea nguvu na weledi katika utendaji kazi wake.
Pia, katika kuendelea kuwainua vijana, wanawake na watu wenye ulemavu Bi Zuwena amesema kwamba ni vyema wataalamu kushirikiana na madiwani kufanya ukaguzi wa kina kwa vikundi vinavyoomba mikopo na kubaini miradi wanayoibua kama ni sahihi na inaweza kusaidia kurejesha fedha watakayokopeshwa ili fedha hizo zirejeshwe kwa wakati na kuendelea kusaidia wanachi wengine.
Katibu Tawala amewasisitiza wataalamu kushirikiana na madiwani kukagua vikundi kabla ya kupewa fedha, kwani waheshimiwa Madiwani ndio wanaowafahamu wananchi wao na itasaidia kutambua vikundi vyenye uwezo wa kurejesha kwa wakati.
Aidha, ametoa pongezi kwa Mkuu wa Wilaya, Madiwani, Mkurugenzi na timu yake ya wataalamu kwa kufanikiwa kupata hati safi ya CAG kwa mara nyingine tena, pia amefurahishwa na namna ambavyo watumishi wanashirikiana na madiwani katika kuijenga halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, amesisitiza utulivu na umoja huo uendelee kudumishwa.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.