Nachingwea, Oktoba 26, 2025.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Nachingwea, ndugu Joshua Mnyang’ali, amewataka wasimamizi wasaidizi wa vituo kuhakikisha wanazingatia kanuni, sheria na taratibu zote zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu.

Akizungumza leo wakati wa semina ya mafunzo ya usimamizi wa Uchaguzi iliyowakutanisha wasimamizi wasaidizi wa vituo 1,632, Mnyang’ali aliwaasa wasimamizi hao kuwa vyanzo vya utulivu na si malalamiko au vurugu katika vituo vyao vya kazi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa timu ili kuhakikisha zoezi la uchaguzi linakamilika kwa ufanisi, akiwataka wasimamizi kuhakikisha wanafika vituoni mapema kukamilisha maandalizi kabla ya siku ya kupiga kura.

Pia aliwakumbusha kuwa wao ndio wanaokutana moja kwa moja na wapiga kura, hivyo wanapaswa kutumia lugha nzuri na kuwapa kipaumbele makundi maalum kama wazee, wajawazito na wenye watoto wadogo.
Mnyang’ali alihitimisha kwa kuwataka washiriki wote kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na kuzingatia sheria za nchi, akisisitiza kuwa ufanisi wa uchaguzi unategemea utekelezaji mzuri wa majukumu yao.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.