MCHANGO WA NACHINGWEA KATIKA KUSAIDIA UKOMBOZI NA UHURU WA NCHI ZA AFRIKA
CHIMBUKO NA HISTORIA YA ENEO LA FARM 17
Eneo la Farm 17 lipo umbali wa kilomita zipatazo 34 nje kidogo ya makao makuu ya wilaya ya Nachingwea,barabara inayoelekea kilimarondo,ikipakana na wilaya ya Masasi.
Historia ya Farm 17 inaanzia miaka ya 1947 baada ya vita kuu ya pili ya Dunia, wakati serikali ya wakoloni wa Uingereza iliamua kufuta baadhi ya ajira kwa waliokuwa askari wa vita hiyo na kuamua kuwatafutia ajira Mbadala.
Serikali hiyo ya wakoloni iliamua kuwatafutia ajira kwa kuwakopesha wapiganaji hao fedha na kuanzisha mashamba ya karanga katika maeneo ya Nachingwea kupitia kampuni ya ‘JOHN MOLEM’.
Kupitia mpango huo mashamba 18 yalianzisha na kupewa majina kuanzia mashamba Farm One(1) hadi Farm 18( yaani Farm 1 hadi 18). Hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali mashamba hayo hayakuendelea na waingereza hao kuamua kuondoka na kwenda kuishi Afrika Kusini . Sababu hizo zikiwepo ni kupata Hasara na ghrama kuwa kubwa ya kusafirisha vifaa na Mitambo n.k.
1. KAMBI ZA MAFUNZO YA KIJESHI TANZANIA
Tanzania ilikuwa ikitoa mafunzo ya kijeshi kwa wapigania uhuru tangu miaka ya 1960 hususani baada ya Tanganyika kupata uhuru Desemba 9, 1961. Wapigania uhuru walianza kuingia nchini kwa vipindi tofauti, ama kwa mafunzo au kusafiri kwenda nchi zingine kupata mafunzo na misaada mingine. Kambi ya kwanza iliandaliwa kwa ajili ya wapigania uhuru wa chama cha FRELIMO huko Bagamoyo mnamo 1963. Mwaka uliofuata, ilihamishiwa Kongwa katika Mkoa wa Dodoma. Kambi ya Kongwa ilihudumia vyama vyote vya wapigania uhuru vilipata mafunzo ya kijeshi nchini Tanzania. Mbali na FRELIMO, walijumuishwa ANC, PAC, SWAPO, SWANU, MPLA, ZANU, na ZAPU. Baada ya muda, kwa sababu za kisiasa na kijeshi zililazimisha Serikali ya Tanzania na Kamati ya Ukombozi ya OAU kuweka kambi tofauti kwa vyama tofauti vya ukombozi.
KAMBI YA FARM 17 NACHINGWEA-LINDI
Wakati vita vya ukombozi viliposhika kasi miaka ya 1970, iligundulika kuwa kuna umuhimu wa kuongeza kambi za mafunzo katika maeneo mengine yanayofaa zaidi. FRELIMO ilihamisha kambi yake kwenda Farm 17 huko Nachingwea, ambayo ilikuwa karibu na mpaka wa Msumbiji ambapo vita vya ukombozi vilikuwa tayari vimeanza hivyo Ilikuwa rahisi kwa wapiganaji kwenda Msumbiji kutoka Nachingwea, ambayo ilikuwa kambi kubwa ya jeshi ya JWTZ yenye majengo mengi, chanzo kizuri cha maji, na uwanja wa ndege, hivyo kufanya kambi iwe salama kutokana na uvamizi wa anga. Serikali ya Tanzania ilimjengea nyumba Rais wa FRELIMO, Samora Machel, kwani alikuwa akitumia muda mwingi huko kusimamia mafunzo ya wapigania uhuru wa FRELIMO. Mnamo 1968, Kamati Kuu ya FRELIMO iliunda Kikosi cha Wanawake (O.M.M) na ikatoa miongozo juu ya uajiri na mafunzo yao huko Nachingwea. Hii ilikuwa alama muhimu katika historia ya mapambano ya ukombozi wa Msumbiji kwani, mbali na kuzidisha safu yake ya kijeshi, iliwapatia wanawake uzoefu sawa na wanaume. Miaka tisa baadaye, ZANLA, kwa msaada wa wanajeshi wa kike wa FRELIMO waliofunzwa huko Nachingwea, walipiga shambulio kwenye kituo cha vikosi vya Rhodesia katika mji wa Chipinge. Wakati Msumbiji ilipopata uhuru mnamo
1975, Kambi ya Farm 17 ilitumika kwa mafunzo ya wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Zimbabwe (ZIPA) hadi walipopata uhuru tarehe 18 April 1980.
Viongozi Mbalimbali wapigania uhuru katika Nchi hizo wakiwemo Samora Machel na Robert Mugabe wameacha kumbukumbu ambazo ni muhimu kwa historia ya Ukombozi wa Afrika. Nchi Mbalimbali licha ya Msumbiji na Zimbabwe kutumia eneo hilo kwa ajili ya mafunzo pia viongozi wan chi za Afrika kusini na Angola waliwahi kupita hapa na kupata mafunzo.
Baada ya Nchi hizo kupata uhuru eneo hilo lilikabidhiwa kwa jeshi la Wananchi wa Tanzania (jwtz) kikosi cha 41 na baadaye eneo hilo likakabidhiwa kwa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea.
FURSA ZILIZOACHWA ENEO LA FARM 17.
Ardhi ya kutosha na yenye rutuba ambayo wanachi wengi wanaitumia kwa kulima mazao ya biashara nay a chakula.
Majengo kwa upande wa na majengo mengine mengine yanatumika kwa shule ya sekondari na shule ya msingi.
Kwa upande wa majengo hayo lipo jingo moja ambalo lilijengwa na Raisi Samora kama ngome yake wakati wa vita vya msumbiji. Jengo hilo chini kwa chini kuna barabara yenye urefu takribani kilomita 1 ambayo ilikuwa unatumika na Rais Samora machel aidha ilikuwa kama ngome ya kujificha na maadui wakati wa vita vya msumbiji na wareno.
Pia Eneo hili kuna majengo Mengine ya kumbukizi kama vile:
Ofisi za utawala wakati huo
Maghala ya chakula
Maghala ya silaha
Jiko na kumbi
Nyumba za walinzi na viongozi
ENEO LA KAMBI YA WAKIMBIZI MATEKWE
Eneo hili lilitumika kama kambi la wakimbizi kutoka masumbiji. Kambi lilianzishwa wakati wa harakati ya wananchi wa Msumbiji kutaka kujikomboa kutoka mikononi mwa wadhalimu kutoka Ureno.
Hivyo wananchi wa Msumbiji waliletwa na kuishi hapa Mwanzoni mwa mwaka 1970 wakati vita vinaendelea. Mwaka 1975 baada ya msumbiji kujipatia uhuru wanachi wengi waliamua kurudi katika nchi yao na baadhi waliamua kubaki hapa hapa matekwe hadi hivi leo wapo.
FURSA WALIZOZIACHA MATEKWE KUTOKANA NA KAMBI YA WAKIMBIZI.
Kuna ardhi na yenye rutuba ambayo wananchi wanatumia katika kulima mazao ya chakula kama mahindi, mpunga, mihogo, mbaazi n.k na kwa upande wa mazao ya biashara wanachi wanajikita kulima zao la korosho.
Majengo- yapo majengo yanayotumika kwa kuishi au makazi ya watu na majengo mengine yannatumiika kwa shule ya msingi na shule ya sekondari.
Yapo majengo mengine yanatumika kama ofisi ya kijiji na Zahanati.
Lipo bwawa kubwa la maji na bwawa hili linatumika kwa uvuvi wa samaki na vile vile kuna mradi wa kilimo unaoneshwa na (ASDP) mradi huu wa umwagiliaji umekwisha tumia ths. Million 500 hadi sasa.
Shule ya msingi Majonanga pamoja na majengo ya nyumba za walimu. Hii ni shule ambayo ipo kijiji cha majonanga ambayo ilijengwa ili kutoa huduma ya elimu kwa wakimbizi na wanakijiji na inatumika hadi hivi sasa. Pia Shule ya msingi Matekwe kabla ya kuwa sekondari Ilijengwa pia kusaidia wakimbizi wakati huo.
Kanisa. Hili ni jengo ambalo kwa sasa ni kigango ambacho kilitumiwa na wakimbizi na wanajamii wengine kupata huduma za kiroho. Pia Father Jerome mwanzilishi wa Kanisa na Parokia ya Kilimarondo (Mei, 2021) alisimulia kuwa hata yeye mara moja moja alikuwa anaenda eneo hilo kutoa huduma ya kiroho pia. Na pia alihusika sana kuwasaidia katika huduma hiyo kwa wakati huo kabla ya kuondoka mwaka 1975.
Salumu Mohamed Migomba(Miaka 95) (Mei, 2021). ‘’ Anasema watu walianza kuja hapo Matekwe kwa kuletwa na serikali mwanzoni mwa miaka ya 1960’s. Watu walianza kujenga mji hadi pale miaka ya 1967 alipofika waziri mkuu wa Tanzania wakati huo Mzee Mfaume kawawa kuwaomba wananchi kuwapokea wageni ( Wakimbizi tokea nchi ya Msumbiji ambao wapo katika mapigano ya ukombozi). Wakimbizi wasiopungua 15,000 walifika eneo la matekwe na kutawanywa katika maeneo mbalimbali yaliyoitwa barabara.’’
KUONDOKA KWA WAKIMBIZI NA URITHI ULIOACHWA
Baada ya Nchi ya msumbiji kupata uhuru mnamo tarehe 25. 06. 1975. Serikali yao ilitangaza wakimbizi wote kurudi nchini humo. Wengi walirudi japo inasemekana wengine waliishia njiani na kuanzisha makao mapya na wengine walichanganyika na wanajamii wengine kusini mwa Tanzania. Pia majengo yote yaliachwa na serikali ya Tanzania iliamua kuyahifadhi maeneo hayo kwa kuendeleza huduma zilizokuwa zinatolewa. Hivyo ukiende leo eneo la matekwe utapata historia ya eneo hilo kwa uzuri.
MCHANGO WA NACHINGWEA KWA UJUMLA KATIKA KULETA UHURU NCHI ZA KUSINI MWA AFRIKA
Nachingwea inajivunia kuwa mji wa UKOMBOZI katika kusaidia nchi nyingi kujikomboa na kujipatia uhuru.
Raisi Julius Nyerere wa Tanzania akiwa na wenzake Samora Machel wa maumbiji (katikati) na raisi wa Zambia (kulia) katika kambi ya FRELIMO,Farm 17 , Nachingwea,Lindi mwaka 1972’
Nachingwea kupitia Eneo la Farm 17 Litabaki katika historia ya kuwa mojawapo ya kambi ya Mafunzo ya kijeshi ambayo yalisaidia mafunzo ya wanajeshi wa Nchi za Msumbiji, Zimbabwe, Afrika kusini na Angola. Msumbiji kupitia Frelimo ndio ambao walikaa muda mrefu Kwa kuanzia mwaka 1968 hadi 1975 na baadaye Wanajeshi wa msumbiji kuanzia 1976 hadi miaka ya 1980 baada ya uhuru. Pia Nchi zingine zilizotajwa hapo juu ziliweza kuleta askari wake kwa ajili ya kupata mafunzo katika kambi ya Nachingwea. Mbali na mafunzo ya kijeshi pia Nachingwea ilitoa maeneo mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya kambi ikiwemo uwanja wa ndege nae neo la Kambi ya wakimbizi matekwe.
Kwa sasa Maeneo mbalimbali ya Nachingwea yana kumbukumbu ya wanaharakati hao ikiwemo eneo la MONDLANE MESS ,Shule ya sekondari Farm 17 bila kusahau kuna jumuiya ya watu wa Msumbiji iliyo hai ambayo inajumuisha watu wanaokaa
Nachingwea. Pia Nchini Afrika kusini kuna Chuo cha Nachingwea na kumbukumbu zingine.
N.B.
Tanzania ni makao makuu ya ukombozi wa afrika, Tanzania ilikuwa na jukumu la kipekee katika mapambano ya ukombozi wa Afrika. Tanzania kwa ujumla inachukuliwa kama kitovu, ngome na kiini cha mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika. Mwaka 2003 wazo la utekelezaji wa programu ya urithi lilibuniwa na Tanzania kwa kushirikiana na UNESCO lengo ikiwa ni kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika hasa nchi za Kusini mwa Afrika. Jumla ya Maeneo 255 yanayohusu program hiyo yamebainishwa na yanaandaliwa utaratibu wa kukarabatiwa ili kuhifadhi historia iliyomo.Nachingwea ni mojawapo ya maeneo hayo na imeanza kufaidika kwa kuanza na kuwekewa mabango yanayoonesha majengo pamoja na Vibao kwa sasa. Utafiti Zaidi bado unaenaendelea.
Imeandaliwa na:
FREDY KOMBA
AFISA UTALII (W)
NACHINGWEA
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.