Marie Stopes imefanya matukio muhimu kuadhimisha Siku ya Wanawake katika Wilaya ya Nachingwea, ambapo walitoa huduma mbalimbali kwa jamii kuanzia Machi 6 hadi Machi 8, 2025. Katika siku ya Kongamano la Wanawake, Machi 6, Marie Stopes walishiriki kwa kutoa matibabu bure, elimu ya afya ya uzazi, na majadiliano kuhusu ukatili wa kijinsia. Hii ilikuwa ni sehemu ya jitihada zao za kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango na kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa ukatili.
Siku ya Machi 7, Marie Stopes wamelifanya bonanza la vijana katika Kata ya Kipara Mtua, ambapo walijumuisha burudani, michezo, huduma za afya bure, elimu ya ujasiriamali, na majadiliano kuhusu ukatili wa kijinsia. Bonanza hili lilikuwa ni fursa ya kipekee kwa vijana kujifunza na kuhamasika kuhusu masuala ya kijamii na kiuchumi.
Tarehe 8 Machi, iliadhimishwa kwa kutoa huduma ya afya bure ambapo. Ndg.Denice Simeo - afisa Vijana Shirika Marie Stopes Tanzania amezungumza mbele ya umati wa wananchi, akitoa shukrani na kupongeza kwa ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa jamii. Amesema:
"Tunafurahi kuona matokeo ya jitihada zetu zinazowawezesha wananchi wa Nachingwea kupata huduma muhimu za afya na elimu. Ushirikiano wa jamii unaleta mafanikio makubwa, na tunaahidi kuendelea kutoa msaada na elimu itakayochangia ustawi wa jamii, hasa wanawake na vijana. Shukrani pia kwa Ofisi ya Mkurugenzi kupitia Idara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano wao mkubwa. Tunaamini hii ni hatua muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi wa Nachingwea."
Wananchi wa Nachingwea walieleza furaha yao na shukrani kwa Marie Stopes, wakisema kuwa huduma zilizotolewa zimewasaidia sana katika kuboresha maisha yao, hasa katika maeneo ya afya, ujasiriamali, na kuelimika kuhusu haki zao za kijinsia. Walisisitiza matumaini yao kuwa zoezi hili liwe endelevu na liwe na manufaa kwa jamii yote, hasa vijana na wanawake.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.