Naibu Waziri wa kilimo Mheshimiwa Omari Mgumba amesema wakulima wote wanaostahili kulipwa fedha zao za korosho watalipwa kabla ya tarehe 31 Mwezi Machi mwaka huu.
Hayo aliyasema jana jioni alipokuwa akiwahutubia wakulima na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mbondo,Kata ya Mbondo, Tarafa ya Kilimarondo.
Alisema kuwa zoezi la uhakiki limekamilika, baadhi ya wakulima wamelipwa ambapo mpaka sasa zaidi ya bilioni 524 zimelipwa kati ya bilioni 700 zilizotakiwa kulipwa.
“Lengo la uhakiki ni kutambua wakulima tulio nao na uwezo wa uzalishaji ili Serikali iweze kuwasaidia kwa mambo mbalimbali ikiwemo mikopo kutoka Benki ya wakulima” Aliongeza Mheshimiwa Mgumba.
Alisisitiza kuwa mamlaka zinazohusika ziweke kwenye mbao za matangazo majina yote ya wakulima waliolipwa ili kuepusha upotoshaji unaondelea wa baadhi ya watu wanaodai hawajalipwa ikiwa wameshalipwa.
Alisema kuwa Serikali inasikitika kwa changamoto zilizojitokeza wakati wa uhakiki lakuni lengo la Serikali ilikuwa ni kumsaidia mkulima aweze kunufaika na kazi zake.
Mapema wakieleza kero zao kwa Naibu Waziri, wakulima walisema kuchelewa kwa malipo kumesababisha washindwe kuandaa mashamba kwa wakati.
Naibu Waziri wa Kilimo yupo kwenye ziara ya kikazi Mkoani Lindi kufuatia maazimio ya kikao kati ya Waziri wa kilimo na Wabunge wa mikoa inayolima zao la korosho , ambapo pia ziara hiyo ina lengo la kuongea na wadau wa sekta ya kilimo.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.