Tunapoelekea kwenye msimu mpya wa uuzaji wa zao la ufuta mwaka 2025, Mkoa wa Lindi unakadiria kuvuna na kuuza jumla ya tani 78,189.5 za ufuta, kwa mujibu wa tathmini ya hali ya hewa ya mwaka huu.
Katika kiwango hicho, Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kimepanga kununua na kusambaza tani 43,987, wakati chama cha RUNALI kinatarajia kukusanya tani 34,202.5.
Maghala yanapangwa kuanza kazi rasmi tarehe 1 Juni 2025, huku mnada wa kwanza ukitarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hiyo hiyo, kulingana na kiwango cha ufuta kitakachokuwa kimewasilishwa kwenye maghala makuu.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, katika kikao cha maandalizi kilichofanyika Mei 22, 2025, ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya ushirika pamoja na mamlaka za serikali kuendelea kusimamia ubora wa zao hilo ili kuwezesha minada kufanyika kwa mafanikio na wakulima kunufaika na bei ya ushindani.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia uchumi na uzalishaji, Mwinjuma Mkungu, ameeleza kuwa Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na Kampuni ya Rotai tayari wamethibitisha ubora wa mizani za kisasa zitakazotumika kwenye mizani ya zao la ufuta.
Aidha, amebainisha kuwa kwa misimu mitano iliyopita, uzalishaji wa ufuta mkoani hapa umekuwa ukiongezeka kutokana na utekelezaji wa mfumo rasmi wa mauzo, ambao umeimarisha ushindani wa bei, kuongeza tija kwa mkulima na kuchangia mapato ya Taifa.
#Tupovizuri
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.