Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, ametoa ahadi ya muda mfupi ya kuwapatia leseni wachimbaji wadogo wa madini katika Mgodi wa Ntaka Hill uliopo katika kijiji cha Nditi Wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi, hayo ameyasema leo Julai 8, 2025 alipokua akiongea na wachimbaji wadogo kijijini hapo.
Mheshimiwa Mavunde amesema kuwa Mheshimiwa Raisi Dkt.Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwarasimishwa na kuwapa Leseni wachimbaji wadogo katika eneo la nditi lenye ukubwa wa hekari za mraba 3.99 na kufungua shughuli za uchimbaji ziendelee katika mgodi huo.
Akizungumza mbele ya mamia ya wanachi katika mkutano huo, Mheshimiwa Mavunde amesema "Serikali imesikia kilio cha wachimbaji wadogo na inalenga kutatua kwa vitendo, kwa kuhakikisha wanapewa leseni haraka ili waweze kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria".
Aidha, amesema "sekta kwa kushirikiana na shirika la madini la serikali (STAMICO) wamejipanga kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata mashine za kuchorongea ili kuweza kurahisisha shughuli za upatikanaji madini", pia ameagiza kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Nachingwea kuhakikisha hakutokei migogoro kwa wenye maeneo yaliyopo ndani ya mgodi kati ya wachimbaji na wananchi.
Kwa upande wao Wachimbaji wadogo wakiongozwa na bi. Kuruthumu Lunje wameelezea furaha na matumaini makubwa baada ya kauli hiyo ya Waziri, wakisema wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata leseni ili wafanye kazi bila hofu ya kusumbuliwa na mamlaka.
Ahadi hiyo ya Waziri Mavunde imezidi kuimarisha imani ya wachimbaji wadogo kwa serikali, huku wengi wakitazamia mabadiliko chanya yatakayobadilisha maisha yao kiuchumi kupitia sekta ya madini.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.