Mhandisi Chionda A. Kawawa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, amewataka Maafisa wa Maendeleo ya Jamii kujikita katika kuwajenga wananchi katika masuala ya kuinua uchumi wao binafsi na kuunga mkono miradi ya maendeleo. Hayo ameyasema alipokuwa katika kikao na Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Halmashauri hiyo, Oktoba 6, 2024.
Mhandisi Kawawa ametoa wito kwa idara hiyo kuwaonesha wananchi jinsi wanavyoweza kutumia fursa zilizopo Nachingwea na kujiinua kiuchumi. Lengo ni kuona wananchi wa Nachingwea wanaendana na fursa mbalimbali zilipo wilayani humo kama mazao ya korosho, ufuta, mbaazi, na fursa za madini. Aidha, mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani imeruhusiwa kutolewa, hivyo Idara hiyo inapaswa kuhakikisha wanasimamia vizuri taratibu mpya za utoaji wa mikopo hiyo. Halmashauri ya Nachingwea imetenga zaidi ya shilingi milioni 939 kwa ajili ya mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Uchaguzi ndugu Robert Mmari aliwahimiza maafisa hao wa Maendeleo ya Jamii kuhamasisha wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, kwa kujiandikisha kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba 2024, na kujitokeza kupiga kura tarehe 27 Novemba 2027.
Aidha, Mhandisi Kawawa alisema kuwa wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali. Maafisa wa Maendeleo ya Jamii wanapaswa kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa elimu ya kutosha ili waweze kujitoa kwa dhati kufanikisha miradi hiyo.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.