Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Mhandisi Chionda A Kawawa tarehe 16 Agosti 2025 alifanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kata na vijiji tofauti ndani ya wilaya hiyo, miradi hiyo inahusisha sekta za afya, elimu pamoja na miundombinu ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha huduma kwa wananchi
Katika ziara hiyo Mkurugenzi alitembelea ujenzi wa Kituo cha Afya Chiola, Zahanati ya Chingunduli, pamoja na ujenzi wa madarasa 3 na matundu 12 ya vyoo katika Shule ya Msingi Majogo iliyopo Litula, aidha alikagua mradi wa TRC Mnero Miembeni, ukamilishaji wa maabara katika Shule ya Sekondari Nditi, pamoja na ukamilishaji wa nyumba ya mganga katika Kituo cha Afya Lionja.
Mkurugenzi alitembelea eneo la Ruponda litakalojengwa Kituo cha Afya, pamoja na shule za msingi Namanja na Ngunichile ambapo miradi ya ujenzi wa madarasa na vyoo inatarajiwa kuanza hivi karibuni, katika Shule ya Msingi Ngunichile mradi huo utahusisha ujenzi wa madarasa 5 na matundu 6 ya vyoo, katika maeneo yote aliyotembelea Mkurugenzi aliwataka watendaji kuhakikisha wanasimamia kwa karibu ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa miradi hiyo, sambamba na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora
Ziara hii imeonyesha dhamira ya dhati ya Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea chini ya Mhandisi Chionda katika kusimamia maendeleo na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki, kupitia utekelezaji wa miradi hii inatarajiwa kuboreshwa kwa kiasi kikubwa huduma za elimu, afya na ustawi wa jamii katika maeneo mbalimbali ya wilaya.
Kwa ujumla miradi yote iliyotembelewa ina thamani ya Shilingi 1,510,981,415/=, jambo linalodhihirisha jitihada kubwa za Serikali katika kuhakikisha wananchi wa Nachingwea wanapata huduma bora na za uhakika.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.