Tarehe 14 Mei 2024 Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Mohamed Hassan Moyo, ametoa wito kwa jamii kurejea kwenye misingi ya maadili, utamaduni na heshima katika malezi ya watoto, akisisitiza umuhimu wa malezi jumuishi bila ubaguzi wa kijinsia.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Familia kiwilaya yaliyofanyika katika ukumbi wa Gunners, Mhe. Moyo amesema jamii ya sasa inapaswa kujifunza kutoka kwa vizazi vilivyopita ambapo watoto walilelewa na jamii nzima kwa pamoja. “Lazima tuimarishe heshima ya mtoto na mzazi, tusibague watoto wa kiume au wa kike – wote wanahitaji malezi bora,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Mhandisi Chionda Kawawa, amesema licha ya jitihada zilizopo, bado maadili miongoni mwa watoto yanazidi kudorora. “Wazazi wa zamani walitulea kwa maadili hata bila elimu kubwa, kwa nini sasa iwe changamoto?” alihoji.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya, Bi. Christina Makula, ameonya kuhusu kuporomoka kwa maadili katika familia, akisema migogoro ya kimya kimya imeathiri vibaya malezi. “Ndoa nyingi leo hazina mawasiliano wala mshikamano – hali inayowafanya watoto kukua bila upendo wala nidhamu,” alieleza.
Maadhimisho hayo yamelenga kuhamasisha wazazi na jamii kwa ujumla kuwajibika katika kujenga familia zenye misingi imara ya maadili, heshima na mshikamano.
#Tupovizuri
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.