Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo, ametoa tahadhari kuhusu mwenendo wa mvua kutokuwa mzuri kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Amesema kuwa kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), maeneo ya Wilaya ya Nachingwea yanatarajiwa kupata mvua za wastani au chini ya wastani.

Ameyasema hayo leo, Februari 19, 2026, alipokuwa katika Mkutano wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC). Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiwango cha mvua kinatarajiwa kuwa kati ya milimita 940 hadi 1000 kwa msimu, huku kukiwa na uwezekano wa baadhi ya maeneo kupata mvua chini ya milimita 940, hali itakayokuwa chini ya wastani.

Taarifa iliyotolewa na TMA inaonesha kuwa hali hiyo inaweza kuathiri uzalishaji wa mazao, hasa mazao ya biashara kama ufuta, mbaazi na korosho katika Wilaya ya Nachingwea. Kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa Moyo amewataka viongozi wa ngazi za kata kuhakikisha wanashirikiana na wataalamu wa kilimo kutoa elimu kwa wakulima ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Moyo ameendelea kukumbusha na kusisitiza umuhimu wa elimu kwa watoto. Amesema kuwa moja ya haki muhimu ya mtoto ni kupata elimu, na kusisitiza kwa wazazi kuwa ni wajibu wao kuhakikisha watoto wanapata elimu. Aidha, amewataka viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa na machifu kuhakikisha watoto wote wanaostahili kwenda shule wanakwenda. Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na miundombinu mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kujifunzia. Aliongeza kuwa elimu ni msingi wa ustawi wa mtoto na taifa kwa ujumla.
Sambamba na hilo, Mheshimiwa Moyo amekumbusha umuhimu wa maadili katika malezi ya watoto na kuhimiza malezi yenye usawa bila upendeleo wa kijinsia, akisisitiza kuwa watoto wote wana haki sawa na ni mhimili wa familia na taifa.
Aidha, amesihi wakazi wa Wilaya ya Nachingwea kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo wilayani humo, ikiwemo kilimo, mifugo na hasa sekta ya madini, ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, wilaya na taifa kwa ujumla. Pia amewataka wakulima wenye mashamba katika maeneo yenye madini kutouza ardhi yao kiholela.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.