Zao la ufuta kumneemesha mkulima
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mheshimiwa Rukia Muwango amewahakikishia wakulima kuwa mfumo wa kukusanya na kuuza zao ufuta kwa njia ya mnada ni bora na yenye tija kwa mkulima
Ameyasema hayo mwanzoni mwa juma wakati akifungua kikao cha wadau wa zao la ufuta katika ukumbi wa Mondlane ambapo kikao hicho kilihusisha viongozi wa vyama vya msingi,maafisa kilimo wa kata, watendaji wa kata waheshimiwa madiwani na baadhi ya wakulima kutoka wilaya ya Nachingwea.
“Kupitia mfumo huu mkulima atalipwa kulingana na bei ya soko,mpango huu una lengo la kumkomboa mkulima kutoka kwa wale wote wenye lengo la kumnyonya” Alisema mheshimiwa Muwango
Akiwasilisha mada katika kikao hicho Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Rafael Ajetu amesema kuwa ufuta utakuwa ukikusanywa kupitia maghala ya AMCOS husika na minada tafanyika katika maghala yaliyoteuliwa ambapo kwa wilaya ya Nachingwea yapo 34.
”AMCOS zitakuwa na jukumu la kujua na kutoa takwimu za kiasi cha ufuta ulioko katika eneo lake mfano ufuta uliokusanywa katika kila tawi na kuziwasilisha kwa afisa ushirika” Alisisitiza Ajetu
Aidha wadau walionesha hofu ya AMCOS kupata hasara na hatimaye baadhi ya wafanyakazi wake kuingia matatani kutokana na unyaufu wa wa zao la ufuta kuwa juu
Akitoa ufafanuzi Mkuu wa Idara ya Kilimo Umwagiliaji na Ushirika Rafael Ajetu amesema kuwa kama ufuta umekauka vizuri hauwezi kupungua uzito kwa haraka na kuwahamasisha wakulima kukausha ufuta wao vizuri kabla hawajaupeleka kwenye maghala ya kukusanyia
Mnada kwa zao hili la ufuta unategemewa kuanza tarehe 12.06.2018, bei yake haitakuwa chini ya shilingi 1764 kwa kilo.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.