Wananchi wa Kiegei B kata ya Kiegei wameridhia ushauri kutoka kwa Mkuu wa divesheni ya utawala wa Halmashauri ya Nachingwea Bi. Rachel E. Lububu wa kuacha tabia ya kususia shughuli za maendeleo ikiwemo Ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho.
Bi. Rachel Erasto Lububu ametoa ushauri huo aliposhiriki Mkutano Mkuu wa Kijiji hicho wenye ajenda kadhaa ikiwemo usomaji wa taarifa za mapato na matumizi , hatua ya Ujenzi wa Zahanati ya kijiji na hali ya uongozi wa Kijiji hasa upande wa Mtendaji.
katika kikao hicho wananchi walieleza changamoto mbalimbali zinazopelekea wao kususia kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo kukosekana kwa taarifa za mapato na matumizi na ushirikishaji wa wananchi katika kufanya maamuzi.
Baada ya kusikiliza wananchi na viongozi wa kijiji hicho Bi, lububu amemtaka Mtendaji wa kijiji hicho kujenga Utamaduni wa kusoma taarifa za mapato na matumizi na kuwaahidi wananchi kuwasiliana na mkaguzi wa ndani kuja katika Kijiji hicho kufanya ukaguzi wa mahesabu ya fedha zote .
Aidha, ametoa wito kwa watendaji wote kuacha tabia ya kutumia fedha mbichi na kujenga Utamaduni wa kusoma taarifa ya mapato na matumizi na kuwataka wananchi kuendelea na Ujenzi kwani kutoshiriki ni kujichelewesha wenyewe ambapo wananchi wameridhia .
Kwa upande wao wananchi wamemshukuru kiongozi huyo kwa kuwakutanisha na kutatua changamoto hiyo na kuanza Ujenzi wa Zahanati .
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.