Wananchi wampongeza Rais Magufuli
Wananchi wa Wilaya ya Nachingwea wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kununua korosho baada ya wafanyabiashara kuonesha kusuasua katika ununuzi.
Wakizungumza leo kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kijiji cha Mkumba wamesema uamuzi huo ni kishujaa na wa aina yake na kuwa anapaswa kuungwa mkono
“Nampongeza sana Rais Magufuli kwa kutunasua sisi wakulima kwani hali ilikuwa mbaya, korosho tulishapeleka ghalani na tulikuwa tunategemea kupata fedha kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za maisha ikiwemo maandalizi ya kuwapeleka watoto sekondari mwakani” Alisema Veronica Makotha mkulima wa korosho
“Sisi wakulima tuna imani na Rais wetu kwani hayumbishwi na mtu yeyote, tunampongeza sana na tunaamini waliochini yake watafanya kila linalowezekana ili wakulima waweze kupata malipo yao kwa wakati” Aliongeza Mkulia mkulima
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha RUNALI kinachohudumia wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Liwale , Hassan Mpako amesema hatua inayoendelea sasa ni kuhakiki majina na akaunti namba za wakulima kwa kushirikiana na maafisa ushirika na kilimo zilizowasilishwa kutoka kwenye vyama vya msingi ili malipo yaweze kufanyika
Aidha ameeleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo usahihi wa majina na akaunti namba za wakulima na kuwataka wakulima wanapopeleka mzigo ghalani waende na vitambulisho vya benki ili kuepuka changamoto hizo.
Ununuzi wa korosho unaendelea kufuatia agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Jumatatu wiki hii wakati akiwaapisha Viongozi mbalimbali aliowateua la Serikali kununua korosho zote za wakulima kwa shilingi 3300 kwa kilo.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.