Wananchi wa Mitumbati wapongezwa kwa ujenzi wa shule ya Sekondari
Wananchi wa kata ya Mitumbati wamepongezwa kwa kuanza ujenzi wa shule ya sekondari ya kata yao na kupunguza adha ya umbali ya watoto waliokuwa wakitembea kutoka Mitumbati kwenda Nangowe ilipo Shule ya Sekondari Kipaumbele
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mheshimiwa, Hashim Komba aliposhiriki kwenye shughuli za kujitolea ambapo wananchi walishiriki kwa wingi kujitolea.
“Mlipoanza safari hii nilidhani ingeweza kuishia njiani lakini mmekwenda na kasi ya ajabu, jingo lote hili lote mnaloliona nguvu ya wananchi ni zaidi ya asilimia 75” Alisema Mheshimiwa Komba.
Aidha, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya amekabidhi bati 35 ikiwa ni sehemu ya bati 70 alizoahidi alipotembelea shule hiyo ambapo aliambiwa baada ya halmashauri kusaidia mabati kulikuwa na upungufu wa bati 70.
“Siku moja nilimuona mwanafunzi mmoja tena alikuwa wa kike mvua inanyesha anaendesha baiskeli shati lake lote limejaa matope niliumia sana, siku moja nilifanya ziara hapa nikakutana na watu wachache nikaahidi nitaleta sabini, leo nimeleta bati 35 ijumaa ijayo nitaleta mengine 35 kufikia 70” Aliongeza Mheshimiwa Komba.
Wanafunzi wa kata ya Mitumbati wanasoma shule ya Sekondari Kipaumbele umbali wa zaidi ya kilomita tano kupata elimu ya sekondari.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.