Wakulima waaswa kuwa watulivu wakati zoezi la uhakiki likiendelea
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mheshimiwa Rukia Muwango amewataka wakulima wilayani humo kuwa watulivu wakati zoezi la uhakiki wa wakulima wa korosho ukiendelea ili kubaini wakulima halali wanaotakiwa kulipwa kutokana na jasho lao ukiendelea.
Mheshimiwa Muwango ameyasema hayo leo wakati akiongea na wananchi wa Kata ya Ngunichile katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ngunichile, Kijiji cha Ngunichile.
“Wananchi muwe watulivu muda si mrefu malipo yatakamilika kwa wakulima wanaostahili kulipwa fedha zao” Amesema Mheshimiwa Muwango
Amesema kuwa nia ya Serikali kununua korosho ni nzuri na ina lengo la kumsaidia mkulima ili aweze kunufaika na jasho lake na kuona harubuniwi watu wasiowatakia mema wakulima hao.
“Mpaka sasa uhakiki umefanyika kwa vyama vya msingi 29 kati ya 36 na zoezi la uhakiki linaendelea, baadhi ya wakulima wamelipwa hadi kufikia tarehe 30.11.2018 wakulima 3500 wameshalipwa fedha kupitia akaunti zao” alisema Mheshimiwa Muwango.
Amefafanua kuwa kwa wale watakaoshindwa kuthibitisha uzalishaji wa korosho zao hawatalipwa, korosho hizo zitataifishwa na kuwa mali ya serikali, kwani wapo wafanyakazi, wafanyabiashara ambao pia wamejihusisha na biashara ya ‘choma chaoma’
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.