TASAF yawakwamua wananchi wa Nachingwea kiuchumi
Walengwa wa kaya masikini wa Kijiji cha Naipanga wilaya ya Nachingwea wameishukuru serikali kwa kuanzisha mradi wa TASAF wa kusaidia kaya masikini
Wakishudia namna walivyonufaika na mradi wa kunusuru kaya masikini mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika jana Bi Zainabu Matola na Bibie Juma walieleza kuwa mradi huo umewakwamua kimaisha
“Niweza kujenga nyumba ya vyumba viwili kuanzisha mradi wa kufuga kuku na biashara ya samaki ambapo faida inaniwezesha kuendesha maisha yangu na familia kwa ujumla” Alisema Zainabu Matola Mkazi wa Kijiji cha Naipanga.
“Kwa upande wangu nimefanikiwa kujenga nyumba ya vyumba viwili kupitia mradi huu, kwa kweli mradi huu umenikomboa sana kwani nilikuwa nalala kwenye nyumba mbovu sana” Aliongeza bi Bibie Juma
Wameeleza kuwa kila walipokuwa wakipata ruzuku, sehemu ya fedha hizo wamekuwa wakizitunza kama akiba na kiasi kilichobaki kutumika kwa matumizi ya kawaida ya familia zao.
Kwa upande wake Mheshimiwa Waziri George Mkuchika amesema TASAF awamu ya tatu inahudumia asilimia 70 ya vijiji Nchi nzima.
“Tunataka wote wanaostahili kupata fedha,hakutakuwa na mtu wa kusema mimi na huyu tumezaliwa mwaka mmoja lakini sijapata, TASAF awamu ya tatu B itafikia vijiji vyote na watu wote wenye mahitaji” George Mkuchika
TASAF awamu ya tatu mpango wa kunusuru kaya masikini unanufaisha vijiji 69 kati ya vijiji 127 wilaya ya Nachingwea.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.