Moi waweka kambi Nachingwea kuwasaidia watoto wenye vichwa vikubwa
Jopo la madaktari kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) limeweka kambi katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea ili kuwapa tiba watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Madaktari wa MOI wameweka kambi katika wilaya hiyo kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Kambi hii ni mafanikio ya kampeni aliyoanzisha Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango.
Akizungumza wakati huduma hizo zikitolewa hospitalini hapo, Muwango, aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wenye matatizo hospitalini ili wakatibiwe.
Alisema kwamba mpaka sasa watoto 15 wameshafikishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu na mpaka jana, saba walikuwa wamefanyiwa upasuaji.
“Kuna watoto wengi wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wilayani hapa na sasa kwa sababu kuna madaktari kutoka MOI, tujitokeze kwa wingi kupata matibabu,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba hospitali hiyo imekuwa ni kituo ambacho madaktari bingwa kutoka Moi wanakitumia kwa ajili ya matibabu ya wenye matatizo hayo.
Muwango alisema kampeni hiyo ya kuwasaidia na kuwafichua watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, ilianza Machi Mosi na ilihitimishwa Aprili 10 kwa ajili ya kuanza matibabu ya upasuaji.
Alisema miongoni mwa sababu za kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye matatizo hayo wilayani humo, ni watoto wa kike kuzaa wakiwa na umri mdogo.
Meneja Uhusiano na Ustawi wa Moi aliyeongozana na madaktari hao, Jumaa Almasi alisema kwamba tatizo la watoto wenye vichwa vikubwa kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara ni kubwa ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.
Takwimu za MOI, zinaonyesha kuwa kati ya watoto 872 waliofanyiwa upasuaji mwaka jana, theluthi moja wanatokea mikoa ya Kusini ikiwamo ya Mtwara na Lindi.
Hivi karibuni, Almasi alikaririwa na gazeti hili akisema kwamba kati ya watoto 19 waliofanyiwa upasuaji katika siku za karibuni, 10 walitokea kwenye mikoa hiyo na tisa katika mikoa mingine nchini.
Mmoja wa wazazi ambao mtoto wake amepata matibabu, Rahel Mhagama kutoka katika Kijiji cha Mgazini, Songea alisema kwamba upatikanaji wa huduma hizo katika Hospitali ya Nachingwea umeleta nafuu kwani awali, alishauriwa ampeleke mtoto wao Hospitali ya Muhimbili. (Chanzo: Gazeti la Mwananchi )
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.