MKUU WA MKOA WA LINDI AWATAKA WAKULIMA KUTUMIA FEDHA ZAO VIZURI
“Tumieni fedha mlizozipata kutokana na mauzo ya korosho kuboresha maisha yenu, Korosho ioneshe kweli maisha yenu yanabadilika na sio kutumia katika mambo ambayo hayana tija kwenu”Alisema mheshimiwa Zambi
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi ameyasema hayo katika siku ya Bonanza la Mkulima wa Nachingwea lililofanyika katika viwanja vya Sokoine Mjini Nachingwea mwishoni mwa juma
Akitoa ushuhuda namna zo la korosho lilivyoboresha maisha yake mkulima ndugu Said Mtalala alisema zao la korosho limeweza kumfanya akanunua matrekta mawili ndani ya msimu mmoja wa kilimo kitu ambacho mfanyabiashara wa kawaida hawezi kufanya.
Aliongeza kuwa matrekta hayo anayatumia kama cha kubebea mizigo yake na kuwakodishia wananchi kubebea mizigo mbalimbali na pia analitumia kulima mashamba yake na wakulima wenzie.
“Kuna watu walikuwa wananicheka wakati nikihangaika na kulima sasa hivi wanavyoona mafanikio yangu wanatamani nao kuanza kulima kwani wameona kilimo kinalipa” Alisema Mtalala
Pia amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muunngano wa Tanzania Mheshimiwa John Magufuli kwa kuboresha bei ya zao hilo na kuondoa tozo zilizokuwa zikimkandamiza mkulima na hivyo kumfanya asione manufaa ya zao hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa amewataka wakulima wengine kuiga mfano wa Mtalala ambaye ametumia fedha zao la korosho kuboresha maisha yake na kupanda kutoka mkulima mdogo na kuwa mkulima wa kati
Aidha Mkuu wa Mkoa amezungumzia kuboreshwa kwa barabara za Masasi hadi Nachingwea ambayo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, barabara ya Nachingwea hadi Nanganga upembuzi na usanifu wa kina umefanyika serikali inatafuta fedha ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wa barabara ya Nachingwea hadi Ruangwa upembuzi na usanifu wa kina umeshafanyika kinachofanyika sasa serikali inatafuta fedha shughuli za ujenzi kwa kiwango cha lami uanze, barabara ya Nachigwea hadi Liwale itafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.