Tarehe 20 Machi, Mh. Adnan Mpyagila, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nachingwea, amefanya ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa shule za sekondari. Ameangalia ujenzi wa Shule ya Sekondari Kata Mtua ,Kata Chiumbati, Rugwa Boys (mabweni), Shule ya Kata ya Nachingwea, na Shule ya Naipanga Sekondari, ambapo amefuatilia maendeleo ya uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Mh. Mpyagila ametoa shukrani kwa Mhe. Rais kwa kuleta fedha nyingi katika sekta ya elimu katika wilaya ya Nachingwea. Amewataka wazabuni kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati ili watoto waweze kuripoti shule mpya na vifaa vipelekwe kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Aidha, Mh. Mpyagila amewahimiza wazazi ambao bado hawajawaleta watoto wao kujiunga na shule za sekondari, hususan wanafunzi wa kidato cha kwanza, kuhakikisha wanaripoti kwa wakati ili waweze kupata fursa ya masomo na kufaidika na uboreshaji unaofanywa katika sekta ya elimu wilayani. Alisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maendeleo, na ni muhimu kwa watoto kujiunga na shule kwa manufaa ya familia na jamii kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, Mwalimu Jonas Joas, Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Nachingwea, amesema imepokea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya shule tatu za Sekondari zinazoendelea kujengwa , Shule ambazo zitasaidia kupunguza umbali mrefu wanaotembea wanafunzi. Alieleza kuwa changamoto za ucheleweshaji wa miradi zimetokana na wazabuni kujiondoa kwa sababu ya mtaji mdogo na usimamizi duni. Hata hivyo, alisema kuwa uandikishaji wa wanafunzi umefikia asilimia 94, huku wakiendelea kukabiliana na changamoto za uandikishaji katika maeneo yenye umbali mrefu.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.