Madawati ya malalamiko kuanzishwa kila kata
Kata zimetakiwa kuanzisha madawati ya malalamiko katika maeneo yao ili kuwafikia wananchi na kutatua kero zao kwa wakati na kupunguza malalamiko miongoni mwa jamii.
Kuundwa kwa madawati hayo kutaondoa madukuduku ya muda mrefu waliyo nayo wananchi na kukosa viongozi wa kuwapelekea kwa utatuzi na kupelekea kuwasubiri viongozi ngazi ya wilaya, mkoa au taifa kwa utatuzi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Namikango jana , Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Hashim Komba amewataka viongozi wa kata baada ya kuunda madawati hayo waandae ratiba na kuisambaza katika katika vijiji ili kuwawezesha wanachi kujitokeza kwa wingi.
“Mwananchi anaweza kuwa na kero yake akienda kwa mtendaji wa kijiji hapati msaada, akienda kwa mtendaji wa kata hapati msaada nap engine watumishi hao hawaishi katika maeneo yao ya kazi, hivyo mwananchi anakata tama na kubaki na dukuduku moyoni mwake madawati hayo yatakuwa ndio suluhisho” Aliongeza mheshimiwa Hashim Komba.
Aidha, amewataka watumishi kuishi katika maeneo yao ya kazi kurahisisha wananchi kuwapata kwa wakati pale wanapohitaji huduma.
Mkuu wa wilaya amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wanaogeuza ofisi zao kuwa sehemu ya mapokezi pale wanapopelekewa shida na wananchi kwa kuwaandika barua na kuwaambia waende wilayani.
Mkuu wa wilaya yupo katika ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi ambapo hadi sasa ameshatembelea kata 17 tangu mwezi Novemba.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.