Tarehe 7 Mei 2025, Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi imefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Nachingwea kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo imeonesha kuridhishwa na ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika ziara hiyo, Kamati imetembelea miradi mbalimbali ya sekta ya elimu na afya. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa mabweni shule ya wavulana Rugwa (Rugwa Boys), ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Naipingo, shule mpya ya msingi Mwananyamala iliyopo kata ya Ruponda, ujenzi wa nyumba za waalimu shule ya sekondari Amandus Chinguile iliyoko kata ya Nambambo. Pia walikagua maendeleo ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Naipingo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Lindi, Esau Barnabas, amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Nachingwea kwa usimamizi mzuri wa miradi, akisema imejengwa kwa viwango na inalingana na thamani ya fedha zilizotumika. Alisisitiza kuwa miradi hiyo ni ya kimkakati na ina mchango mkubwa katika kuinua huduma za kijamii hususan elimu na afya.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuitunza miundombinu hiyo na kuhakikisha watoto wanapelekwa shule na kutumia huduma za afya kwa maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla. “Miradi hii ni kielelezo cha utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli. Hivyo ni wajibu wetu sote kuitunza na kuiendeleza,” alisema.
Aidha, amewataka wanaCcm wenye nia ya kuwatumikia wenzao katika nafasi za uongozi kujitokeza kuchukua fomu wakati ukifika, ikiwemo kugombea udiwani na ubunge, ili kuendeleza kazi nzuri inayofanywa na chama na serikali.
#Tupovizuri
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.