Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Chionda Kawawa, amewataka wabanguaji wa korosho kuchangamkia fursa ya mikopo ya mashine za kubangua korosho inayotolewa kwa udhamini wa NMB Foundation na NMB Bank.

Ameyasema hayo leo novemba 13, 2025 katika kongamano lililofanyika ukumbi wa Polisi Mess.
Mpango huo unalenga kuboresha na kuongeza thamani ya zao la korosho kwa kuwawezesha wabanguaji wadogo kuachana na mbinu za asili na kutumia teknolojia za kisasa katika shughuli zao.

Mhandisi Kawawa ameeleza kuwa ofisi ya Mkurugenzi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha vikundi vya wabanguaji vinapata masoko ya uhakika kwa bidhaa zao, sambamba na kuboresha mazingira ya uzalishaji ili bidhaa zinazozalishwa ziwe bora na zenye ushindani mkubwa sokoni.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wabanguaji hao kuwa waaminifu na wabunifu katika matumizi ya mikopo watakayopata ili kuhakikisha inaleta tija kwao binafsi na kwa maendeleo ya wilaya kwa ujumla.

Mhandisi Kawawa pia ameeleza kuwa Wilaya ya Nachingwea inaendelea kufunguka kiuchumi kutokana na fursa mbalimbali ikiwemo uwepo wa madini, hivyo ni muhimu kwa wananchi kujiandaa kunufaika na fursa hizo kwa kuboresha bidhaa na kuongeza thamani ya mazao yao.
Kwa Kupitia ushirikiano kati ya halmashauri, NMB Foundation na wadau wengine wa maendeleo, Nachingwea inaendelea kujipambanua katika uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, hususan korosho, ili kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa wananchi wake.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.