Leo tarehe 5 Juni 2025, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo, amefungua rasmi mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa mwaka 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya Mafuta Ilulu.
Jumla ya vijana 132 wamejiunga na mafunzo hayo kwa lengo la kujiimarisha katika uzalendo, nidhamu, na stadi za kijeshi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mheshimiwa Moyo amesema taifa linahitaji vijana wazalendo, wakakamavu na waadilifu ambao wanaweza kulitetea na kuilinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameahidi kuwa wahitimu wote wa mafunzo hayo watapewa kombati zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 12 ili kuwapunguzia mzigo wazazi ambao wamekuwa wakihamasisha watoto wao kujiunga na jeshi hilo.
Aidha, amewahimiza vijana wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ili waweze kushiriki moja kwa moja katika kuisaidia nchi yao.
Katika kuonesha kuthamini mchango wa vijana hao, Mkuu wa Wilaya ameahidi kuwaletea ng’ombe mmoja kama zawadi maalum, ikiwa ni ishara ya motisha na shukrani kwa kujitolea kwao.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya uzalendo na ulinzi wa taifa miongoni mwa vijana wa Nachingwea.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.