Baraza la madiwani robo ya tatu mwaka wa fedha 2022 /2023 la wilaya ya Nachingwea limefanya mkutano wa baraza baada ya kutanguliwa na vikao vya kamati na uwasilishaji wa taarifa za kata. Katika mkutano huo waheshimiwa madiwani wameweza kujadili maswala kadhaa yanayohusu maendeleo ya wilaya yakiwemo kuchelewa kwa pembejeo za kilimo katika msimu husika ambapo waheshimiwa wamemsisitiza Mkurugenzi kuchukua hatua za makusudi katika kuhakikisha mbolea inawafikia wananchi mapema kupitia idara ya kilimo . Kwa upande wa mkurugenzi. kupitia mkuu wa idara wa kilimo na umwagiliaji ametumia fursa hiyo kuwaomba waheshimiwa madiwani kwakuwa changamoto kubwa ni uhaba wa wazabuni wanaoweza kuchukua mzigo kwa wingi na kuja kuwauzia wananchi kwa bei nafuu, hivyo wavishawishi ama kuvishauri vyama vya msingi kutumia fursa hiyo ya kuchukua pembejeo na kuwauzia wakulima.
Mali na mjadala wa pembe jeo , waheshimiwa madiwani wamejikita hasa katika kutafuta suluhu ya changamoto kuu tatu, ambazo ni namna ya kuwadhibiti tembo na athari zake, Kuomba ufafanuzi wa matumizi ya fedha za mfuko wa elimu na udhibiti wa mapato ya mgodi wa nditi.
Waheshimiwa madiwani wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Lindi kushiriki kikao cha baraza maalum la Halmashauri ya Nachingwea kwa ajili ya ufafanuzi na kujadili matumizi ya fedha za mfuko wa elimu ambao unatokana na makato ya mazao ya biashasra hasa korosho.Waheshimiwa madiwani wamefikia uwamuzi huo kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa la kuzitaka halmashauri za Mkoa wa Lindi kutumia fedha za mfuko wa elimu kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwa ujumla wake na siyo kuzigawa kila kata kulingana na walichochangia.
Akichangia diwani wa kata Marambo Mhe. Selemani Katali amesema kubadilishwa kwa matumizi kwa fedha hizo kunaleta changamoto kubwa kwa wananchi kwani matarajio ya wananchi katika kila kata kuona fedha hizo zinashuka katani kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya ndani ya kata kulingana na kilichochangiwa . Hivyo agizo hilo linahitaji mjadala na ufafanuzi wa kina kuhusu kubadilishwa kwa matumizi .
Mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Adinani Mpyagila aliwaeleza waheshimiwa madiwani kuwa kupitia kikao cha kupitia taarifa za shughuli za maendeleo kwenye kata, makubaliano kuwa aombwe Mkuu wa Mkoa kushiriki baraza maalum kwa ajili ya ufafanuzi wa kubadilishwa kwa matumizi ya fedha hizo. Taarifa hiyo iliungwa mkona wa wajumbe na kuridhia kuombwa kwa mkuu wa mkoa katika baraza hilo.
Kwa upande wa changamoto ya tembo ambayo inaathiri baadhi ya wananchi wa wilaya ya Nachingwea , baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Nachingwea limeiomba serikali kuanza kuitumia helikopta kwa dharura kwa lengo la kuokoa jamii kutokana na uaribifu wa mazao na vifo kwa wananchi.
Akichangia mada ya tembo diwani wa kata ya Ngunichile Mhe. Said Makayola amesema baraza linapaswa kuchukua hatua za haraka katika kutatua changamoto ya tembo kwani hali ni mbaya kwa wananchi.
Kutokana na michango ya waheshimiwa madiwani , Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Adinani Mpyagila akidhibitisha uwepo wa kadhia hiyo, ameiomba serikli kuona umuhimu wa kutumia helikopta kwa dharura kwa lengo la kunusuru jamii, kwani njia hiyo imekuwa msaada wa haraka kwa sasa wakati njia ya kudumu ya kutatua changamoto hiyo inaendelea kuwekwa sawa.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.