WAZIRI MKUU AMEWASHAURI WAKULIMA KUTENGA FEDHA KWA AJILI YA KUNUNULIA MADAWA YA KILIMO KWA MAZAO YAO.
Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewataka wakulima kutenga fedha kwa ajili ya kununua pembejeo kwa ajili ya kuhudumia mikorosho yao kulingana na mahitaji na idadi ya mikorosho mkulima anayoimiliki.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mpiruka leo alipokuwa akielekea jimboni kwake wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi na mapumziko ya mwisho wa mwaka
“Mwaka huu serikali imegawa pembejeo kwa wakulima, hazikutosha kwa wananchi mlikata tamaa, Rais amewapa changamoto ili mfufue mikorosho yenu.Kila mtu ajipange kununua madawa kwa ajili ya mikorosho yake kulingana na idadi ya mikorosho aliyonayo.” Mh Majaliwa alisema
Aidha , amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imetenga fedha za kutosha ili kuhakikisha kila kijiji nchini kinapata umeme ambapo pia Kijiji cha Mpiruka ni miongoni mwa vijiji zaidi 30 vitakavyopata umeme kupitia program ya umeme vijijini katika wilaya ya Nachingwea awamu hii .
Akizungumzia suala la upatikanaji wa maji kwa watu wa Kijiji cha Mpiruka amemtaka Meneja wa MANAWASA kupeleka maji kwa watu wa Kijiji cha Mpiruka kwani kero kubwa inayowakabili wananchi wa Kijiji hicho na pia hakipo mbali na Kijiji cha Mkumba ambapo ndio maji yapoishia kwa sasa.
Pia aliwaasa wananchi kutokata miti hovyo na kuharibu vyanzo vya maji,kwa kukata miti hovyo kunasababisha ukame na watu kuhangaika kwa kukosa maji.
Mapema akieleza kero za wananchi wa Jimbo la Nachingwea husani kata ya Mpiruka Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mheshimwa Hassan Masala ameishukuru Serikali kwa kuwapatia wakulima pembejeo na kuomba msimu wa kilimo ujao pembejeo zifike kwa wakati.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Godfrey Zambi amewataka wananchi kuwataka wananchi kuwapeleka watoto wao shule mapema shule zitakapofunguliwa mwezi Januari na mzazi yeyete ambaye hatampeka mtoto shule kwa maana ya darasa la kwanza na kidato cha awali hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Pia aliwataka wananchi kupanda miche mipya ya mikorosho na kuondoa ile ya zamani ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo, amesema serikali itagawa miche ya mikorosho bure na uzinduzi Kiwila utafanyika tarehe 06.01.2018 katika viwanja vya Sokoine kupitia Bonaza la wakulima.
Waziri Mkuu yupo kwenye ziara ya kikazi jimboni kwake na mapumziko ya mwishoni mwa mwaka
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.