WANANCHI WATAKIWA KUSHIRIKI KWA WINGI KATIKA VIWANJA VYA MAONESHO YA NANE NANE NGONGO KUJIFUNZA MBINU MBALIMABLI ZA KILIMO
Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amewataka wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Ngongo kujifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua maonesho ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa kanda ya kusini inayohusisha Mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na wilaya ya Tunduru iliyopo Mkoa wa Ruvuma.
Simbachawene amewataka wakulima kulima kilimo chenye tija kwa kufuata maelekezo ya maafisa ugani walipo katika maeneo yao na kuepuka kuharibu mazingira ili kuepuka mabadiliko ya tabia nchi.
“Wananchi washiriki katika kilimo kila mmoja kwa kupokea tafiti na maelekezo ya wataalam,wafanye kilimo cha kiuchumi,ufugaji wa kiuchumi na uvuvi wa kiuchumi” Alisema Mheshimiwa Simbachawene.
Awali akimkaribisha Waziri Simbachawene Naibu Waziri wa Kilimo ,Mifugo na Uvuvi Ole Nasha amewahakikishia kiasi cha pembejeo kilichotengwa kwa ajili ya zao la korosho zitasambazwa katika maeneo husika kabla ya tarehe 20 mwezi huu.
Kauli mbiu ya maazimisho ya wakulima maarufu kama Nane Nane ni “Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo ili kufikia uchumi wa kati”
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.