Waliohujumu fedha za mauzo ya korosho kukamatwa
Mkuu wa wilya ya Nachingwea Mheshimiwa Rukia Muwango amemuagiza Kamanda wa polisi wa wilaya kuwakamata mara moja wale wote ambao wamehusika na ubadhirifu wa fedha za wakulima na kupelekea wakulima kutopata fedha zao za malipo ya mauzo ya korosho .
Ameyasema hayo jana wakati akiongea na waheshimiwa Madiwani katika kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ulipo mjini Nachingwea.
“OCD nakuagiza kuanzia sasa hivi wale wote wanaohusika katika ubadhirifu huu wakamatwe mara moja na warudishwe mahabusu,kama ni kulipa deni watalipa wakiwa mahabusu nataka ijumaa nije niwasalimie wakiwa mahabusu” Alikazia Mheshimiwa Muwango
Aliongeza kuwa mpaka sasa ni vyama 13 ndio vinadaiwa na wakulima na kesi zipo katika hatua mbalimbali lakini wamekuwa wakipuuza kwa kuwa wanaona kesi hizi ni za madai ndio maana anaamuru wakamatwe mara moja hata kama walishapata dhamana.
Mkuu wa Wilaya ametoa ufafanuzi na maagizo haya baada ya Waheshimiwa Madiwani kuhoji hatua zilizochukuliwa kufuatia baadhi ya wakulima kutopata fedha za mauzo ya korosho na msimu umeshafungwa.
Aidha Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amewaonya viongozi na watumishi kutojihusisha na vitendo vya uhalifu kwani kumekuwa na taarifa ya viongozi na watumishi kujihusha matukio ya uhalifu kama uvunaji haramu wa mazao ya misitu.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.