Leo tarehe 25 Januari 2025,Afisa Mwandikishaji Wilaya ya Nachingwea Mhandisi Chionda Kawawa amefungua mafunzo na kuwaapisha waandishi wasaidizi vituoni na waendesha vifaa vya bayometriki, katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Ualimu (TTC) Nachingwea.
Katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Chionda amewasihi waandishi wasaidizi na waendesha bayometriki kutunza vifaa watakavyopatiwa kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo la uboreshaji, amewasisitiza umuhimu wa ushirikiano, ufanisi, na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao. Aliongeza kuwa, kwa kuwa zoezi hili ni nyeti na muhimu, wanapaswa kuwa makini na kutunza siri zote zinazohusiana na shughuli hiyo.
Aidha, Mhandisi Chionda aliwaomba kuwa na lugha nzuri wakati wa kutoa huduma kwa wananchi, kwani wananchi wanatarajia kupata huduma bora na za kiwango cha juu katika zoezi hili muhimu.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.