VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI VYATAKIWA KUTUMIA MIKOPO WALIYOPEWA KUJIKWAMUA KIUCHUMI
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mheshimiwa Rukia Muwango amevitaka vikundi vya wajariamali kutumia vizuri fedha wanazopewa kama mkopo na Halmashauri ili kujikwamua kiuchumi.
Ameyasema hayo wakati akikabidhi hundi ya shilingi milioni 86 kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na walemavu inayotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri
“Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kunapaswa kuungwa mkono na kila mtu, mnatakiwa kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha hizi kwa kuweka kumbukumbu sahihi za matumizi na kutobadili matumizi yaliyokusudiwa” Aliongeza Mheshimiwa Muwango
Pia amewataka wajasiriamali hao kurejesha fedha hizo kama masharti yanavyoelekeza kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia na wengine kunufaika na fedha hizo kwani zinaenda kwa mzunguko.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kukabidhi hundi hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri amevitaka vikundi hasa vya vijana na walemavu kujitokeza ili kuweza kupata mikopo kwani fedha zipo.
Aidha, akitoa taarifa ya mikopo kwa mgeni rasmi Afisa Maendeleo ya Jamii bi Esther Makomba amesema Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi 283,565,710 kama asilimia kumi ya mapato ya ndani ambayo ni shilingi 2,835,657,099.
Kwa robo ya pili kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba 2017 halmashauri inawakopesha vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na walemavu.
“Halmashauri imelenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuhakikisha fursa ya mikopo kwa ajili ya mitaji inapatikana bila urasimu na masharti nafuu na kuwafikia wananchi wengi, mkikopo hii inapaswa kurejeshwa baada ya mwaka mmoja tangu mkopo ulipotolewa” Alisisitiza bi Makomba
Mikopo yenye jumla ya shilingi 299,000,000 imetolewa na kuwanufaisha wananchi 2,560 katika vikundi 128 kutoka kata 36 za wilaya ya Nachingwea.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.