“Tupo tayari kujitolea kujenga kituo cha Afya Kilimarondo” Wananchi
Wananchi wa Kata ya Kilimarondo wameahidi kujitolea kushirikiana na mafundi ili kuhakikisha mradi wa kujenga majengo yaliyokusudiwa unakamilika kwa wakati na kwa gharama nafuu zaidi.
Wametoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa hadhara wa uhamasishaji uliofanywa na Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mheshimiwa Hassan Elias Masala uliokuwa na lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki katika mradi huo.
“Serikali imeleta Shilingi milioni mia nne kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki cha Kilimarondo, yatajengwa majengo mapya ambapo yakijengwa hata sura ya kituo hiki itabadilika” Alisema Mheshimiwa Mbunge
Akitoa ufafanuzi wa majengo yatakayojengwa, Kaimu Mhandisi wa Ujenzi Hamidu Ngililea ni pamoja na chumba cha wagonjwa wan je (OPD), jengo la upasuaji, maabara, jengo la kujifungulia na chumba cha maiti.
Mheshimiwa Mbunge amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika kutekeleza shughuli zinazowahusu kama ratiba na shughuli husika zitakavyoandaliwa na wataalam ili kupunguza gharama za ujenzi ili fedha zitakzobaki zitumike kwa shughuli nyingine za kuboresha kituo.
“Tukiacha kazi zote tulipe fedha tutashindwa kukamilisha majengo yote tunayoyataka kwani tutajikuta tumetumia fedha nyingi kuliko fedha tulizonanazo, nawaombeni sana tujitokeze kituo hiki ni cha kwetu, mimi nitakuja hapa kushiriki na nyinyi kuchimba msingi na kazi nyingine zisizo za kitaalam” Aliongeza Mheshimiwa Mbunge.
Mradi huu wa ujenzi unatakiwa kukamilika tarehe 31.05.2018 ambapo majengo ya chumba cha OPD, jengo la upasuaji, maabara, jengo la kujifungulia na chumba cha maiti yatajengwa
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.