Serikali ya kijiji cha Nditi, ikiongozwa na Mwenyekiti Salumu Amuli Husseni, ilifika katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea. Lengo la ziara hiyo lilikuwa kuwasilisha kero zinazowakabili wananchi, zikiwemo changamoto katika sekta ya afya, nishati na wanyamapori.
Wakiwa hapo, walikutana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, ambaye pia ni Afisa Mipango, Joshua Mnyang’ali. Mwenyekiti alieleza kuwa wodi ya wazazi katika zahanati ya kijiji haijakamilika, kijiji kinakosa huduma ya umeme, na tembo wamekuwa wakiingia kwenye makazi ya watu na mashamba yao.
Joshua Mnyang’ali aliwapongeza viongozi hao kwa kufuatilia maendeleo ya wananchi wao. Alieleza kuwa suala la wodi ya wazazi tayari lipo kwenye mpango wa utekelezaji na zabuni inatarajiwa kuanza mwezi wa tisa. Kwa upande wa umeme, TANESCO wanatarajiwa kufika kijijini wiki ijayo, na kuhusu tembo, halmashauri imenunua drone kwa ajili ya kuwafukuza.
Aidha, Joshua alieleza kuwa kijiji cha Nditi ni kikubwa na chenye fursa nyingi, hivyo kinahitaji miundombinu madhubuti. Alisema halmashauri itaangalia uwezekano wa kuingiza ujenzi wa Kituo cha Afya katika mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mwisho wa kikao, Mwenyekiti Salumu alitoa shukrani za dhati kwa ofisi ya Mkurugenzi kwa namna walivyopokea hoja zao. Aliomba pia kijiji hicho kitambuliwe rasmi uongozi wake, kutokana na juhudi wanazoendelea kufanya katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.