Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 296 kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la uchanjaji wa mifugo nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kudhibiti magonjwa hatari yanayopunguza tija kwa mfugaji na kuathiri upatikanaji wa soko la kimataifa.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mifugo na Uvuvi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, amesema serikali imepanga kufikia lengo la kuchanja asilimia 70 ya mifugo yote nchini ifikapo Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa takwimu, jumla ya ng’ombe wanaokadiriwa kuwapo katika mikoa ya Lindi na Mtwara ni zaidi ya mifugo laki tatu na ambao nao wanatarajiwa kufikiwa na zoezi hilo, huku ikitarajiwa kuwa miongoni mwa mikoa inayotarajiwa kutekeleza kwa ufanisi zoezi hilo.
“Magonjwa yasipodhibitiwa huathiri kwa kiasi kikubwa thamani ya mifugo katika soko hasa la kimataifa. Serikali imeweka msukumo ili kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi ili kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuleta tija kwa mfugaji pamoja na kudhibiti tatizo la uwizi wa mifugo” alisema Dkt. Mhede.
Vilevile, Dkt. Mhede amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea na mpango wake wa kuwawezesha wananchi kupitia sekta za kimkakati ikiwemo Kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuongeza msukumo ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na sekta hizi za kimageuzi, Katika upande wa uvuvi, serikali inaendelea kuwawezesha wavuvi wa ukanda wa pwani kwa kuwapatia boti za kisasa kupitia mikopo isiyo na riba, ili kuongeza tija katika shughuli zao na kuchochea uchumi wa buluu, na wakulima wakiendelea kunufaika na utolewaji wa pembejeo za kilimo bure.
Aidha, kupitia maadhimisho hayo, Dkt. Mhede amewakumbusha wananchi kuzingatia ulaji wa lishe bora, hasa protini zinazotokana na wanyama, huku akisisitiza matumizi ya bidhaa za mwani kwa afya na tiba, zikiwemo mafuta, unga na mbolea ya mwani pamoja na kuzitaka halmashauri kushirikiana na wataalamu kutoka idara za afya, lishe na maendeleo ya jamii ili kuhakikisha wananchi wananufaika na jitihada hizi za serikali katika kuboresha maisha yao.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.