Tarehe 18 Oktoba 2024, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea Dr Ramadhani Maige, amefungua rasmi mafunzo ya matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoa huduma za afya ngazi ya hospitali na vituo vya afya katika wilaya ya Nachingwea. Mafunzo haya yameandaliwa ili kuwajengea uwezo wahudumu wa afya katika kutengeneza maziwa dawa yatakayosaidia katika matibabu ya watoto wenye utapiamlo mkali.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dr. Maige alisisitiza umuhimu wa wahudumu wa afya kufikia watoto walioko maeneo ya ndani ili waweze kupata matibabu stahiki. “Ni jukumu letu kuhakikisha watoto wetu wanapata huduma bora za lishe na matibabu ili kuondokana na tatizo hili la utapiamlo,” alisema.
Afisa Lishe, Dalahile Zubery Rumisha, ambaye ndiye kiongozi wa mafunzo hayo, alitoa wito kwa watoa huduma hao kujikita katika kuzuia tatizo la utapiaml "tunapaswa kutoa si tu matibabu bali pia elimu juu ya lishe bora ili tuweze kumaliza tatizo la utapiamlo katika wilaya yetu,” aliongeza.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za serikali na wadau wa maendeleo katika kuimarisha afya ya watoto na jamii kwa ujumla, huku lengo likiwa ni kuboresha maisha ya watoto walio katika hatari ya utapiamlo.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.